Beki wa kulia wa klabu ya Inter Milan ya nchini Italia pamoja na timu ya taifa ya Uholanzi Denzel Dumfries ameweka wazi kua bado ataendelea kuwatumikia mabingwa hao wa Italia kwa msimu ujao.
Dumfries ameeleza kua ataendelea kuwepo ndani ya klabu ya Inter Milan kwa siku za mbeleni licha ya kuhusishwa kutimka klabuni, Ambapo vilabu mbalimbali barani ulaya vimekua vikiwinda saini yake haswa vilabu kutoka nchini Uingereza.
“Nadhani mustakabali wangu utakuwa Inter, ndio. Ni klabu ya juu na ninaipenda, ninahisi niko nyumbani Inter.”
“Tuko kwenye mazungumzo kuhusu mkataba mpya, kuna umiliki mpya sasa, tuone kitakachotokea – lakini Inter ni familia yangu, naipenda sana klabu.”
Manchester United ni moja ya vilabu ambavyo vinaelezwa kuwinda kwa karibu saini ya beki huyo wa kulia wa kimataifa wa Uholanzi, Lakini mpaka sasa beki huyo ameweka wazi kua mipango yake ni kuendelea kuitumikia klabu ya Inter Milan vigogo wa soka nchini Italia.Licha ya mazungumzo ya Dumfries lakini bado kuna nafasi kwa vilabu ambavyo vinamtaka mchezaji huyo, Kwani mazungumzo ya mkataba mpya baina yake na klabu ya Inter Milan yanaweza yakakwama vilevile wanaweza kupeleka dau ambalo klabu ya Inter inaweza kua ngumu kukataa.