Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, ameweka jina lake kwenye vitabu vya historia baada ya kushinda tuzo ya PFA Players’ Player of the Year 2024/25, akiwapiku mastaa kadhaa akiwemo Bruno Fernandes na Alexander Isak.

Salah alitangazwa mshindi usiku wa Jumanne katika ukumbi wa Manchester Opera House, na kufanikisha mafanikio ya kipekee kwa kuwa mchezaji pekee katika historia kutwaa tuzo hiyo mara tatu, baada ya mafanikio ya awali msimu wa 2017/18 na 2021/22.
Mshambuliaji huyo kutoka Misri alistahili kutambuliwa kutokana na mchango wake mkubwa msimu uliopita, akihusika kwenye mabao 47 kwa jumla (magoli 29 na asisti 18), akiiongoza Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England.
Katika kinyang’anyiro hicho, Salah pia aliwashinda wagombea wengine waliokuwa kwenye orodha fupi: Declan Rice (Arsenal), Cole Palmer (Chelsea), Alexis Mac Allister (Liverpool), Bruno Fernandes (Manchester United) na Alexander Isak (Newcastle United).

Isak, aliyemaliza akiwa mfungaji bora wa pili nyuma ya Salah na ambaye sasa anahusishwa na tetesi za kutua Anfield, aliwasha moto msimu mzima. Rice aliibuka kuwa nguzo muhimu kwa Arsenal licha ya timu hiyo kushindwa katika mashindano ya ndani na Ulaya, wakati Palmer aliendelea kuvutia kwa ufanisi wake mbele ya lango. Mac Allister, kwa upande wake, alishirikiana vyema na Ryan Gravenberch na Dominik Szoboszlai katika kiungo cha Liverpool, huku Fernandes akiendelea kuwa mwanga pekee katika msimu mgumu kwa Manchester United.
Mbali na Salah, washindi wengine wa tuzo za PFA walikuwa ni Morgan Rogers (Aston Villa) – PFA Young Player of the Year, Mariona Caldentey – Mshindi wa tuzo kuu ya Women’s Super League, James Trafford (sasa Manchester City, zamani Burnley) – Championship Player of the Year.
Tuzo za PFA hutolewa na Professional Footballers’ Association, ambapo wachezaji wa ligi mbalimbali hupiga kura. Mfumo wa kura unahusisha awamu mbili: kura ya kwanza kuunda orodha fupi, na kura ya pili kuamua mshindi. Ni kanuni kuwa mchezaji hawezi kumpigia kura mchezaji mwenzake wa klabu moja.

Huku tetesi nyingi zikimzunguka kuhusu mustakabali wake, Salah aliweka kando mijadala ya nje ya uwanja msimu uliopita na kuendelea kutoa kiwango bora kila wiki kabla ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Anfield. Baada ya kushinda tuzo hiyo kubwa binafsi na kuimarisha mustakabali wake, changamoto inayofuata kwa Salah na Liverpool ni mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Newcastle Jumatatu ijayo, kufuatia ushindi wao wa ufunguzi dhidi ya Bournemouth.


