Ubaguzi Haufai Katika Soka!

Klabu ya Tottenham inaripotiwa wapo katika uchunguzi wa kina juu ya sakata linaloripotiwa kuwa ni ubaguzi wa rangi uliokithiri kwa baadhi ya wachezaji wao. Mashabiki wanatajwa kuwa ni chanzo kikubwa cha suala zima hilo linaloendelea ndani ya klabu hiyo kwa sasa. Hisia za mchezo, imani mbovu au wakati mwingine kutokupenda vitu vinavyofanywa na mchezaji husika huchangia kwa kiwango kikubwa suala zima la kutolewa maneno yasiyo ya kiuungwana uwanjani.

Tumekuwa tukishuhudia mashabiki wa timu nyingine wakiwa ndio watu wa kwanza kabisa kutamka maneno yenye kudhihirisha ubaguzi huo, lakini mambo yanakuwa tofauti kabisa kwa sasa; kwamba mashabiki ndani ya timu hiyo hiyo wanawatamkia maneno ya kashfa na yasiyo ya kiuungwana wachezaji wao.

Klabu ya Tottenham imeanza mchakato wa kufuatilia suala lililojitokeza katika mechi ya mwisho wa wiki kati yao na Manchester United ambapo kikundi fulani cha mashabiki wa klabu hiyo walijuwa wakirusha maneno ya ubaguzi kwa mchezaji wa timu yao Son Heung-Min. Ambapo inasemekana maneno hayo yalikuwa na nia mbaya na kumtukana mchezaji huyo kutokana na taifa lake na rangi yake.

Sio mara kwanza mchezaji huyo kutolewa aina hiyo ya maneno; baadhi ya mashabiki wanadai kwamba amekuwa akifanyiwa hivyo mara kwa mara akiwa uwanjani kitu ambacho kinapunguza sana ari kwa wachezaji. Kwani, mchezaji huhitaji faraja yote ili asitoke mchezoni anapopambania timu yake.

Shirikisho la soka duniani wanajitahidi kupigania suala hili ili kuweza kuondoa chembe zote za ubaguzi katika michezo, lakini juhudi zao zinaangushwa na vitu kama vivi ambapo ni vigumu kupambana na mtu mmojammoja bali ni suala mtanbuka la kila mpenda soka kupambana ili kuhakikisha masuala kama haya yanafikia kikomo kabisa katika soka.

Juhudi za FIFA zinapaswa kuungwa mkono kwa kiwango kikubwa ili kuondoa masuala kama haya; ikiwemo kuwafungia hata mashabiki kutokuonekana viwanjani kama watakuwa wamehusika kwa namna moja au nyingine kwa vitendo hivyo visivyo vya kiuungwana kabisa kimichezo. Maana havipaswi kwa namna yoyote ile kushamiri katika soka na ikitokea vitavunja moyo wachezaji wenye asili fulani.

Na wachezaji wenye asili ya kiafrika huwa ni wahanga wakuu katika hili. Kama alivyofanyiwa hivi karibuni Piere Aubameyang katika kitendo cha kurushiwa ndizi huku mechi ikiwa inaendelea. Vitendo hivi sio vya kimichezo kabisa vyenye nia ya kuvuruga mchezo wa soka, ambao unasemekana kuwa mchezo unaounganisha watu wengi sana duniani. Hivyo, kuna haja ya kujifunza katika mambo haya ili yakemewe kwa sauti moja duniani kote na kuona watu wote ni sawa na wanapaswa kuthaminiwa katika usawa bila kuangalia rangi zao au utaifa wao.

2 Komentara

    Mmh

    Jibu

    Black lives matter play together 😂

    Jibu

Acha ujumbe