“Hatusajili Tena Januari!” – Pep

Mzee wa mipango ya muda mrefu, Pep Guardiola amekiri wazi kwamba hawatazamii kuongeza jina lolote jipya kikosini hapo kwa Januari katika dirisha la usajili akiamini kwamba wachezaji alionao wanatosha kabisa kuleta mabadiliko makubwa kikosini hapo kwa siku za karibuni.

Kikosi hicho kina kila linalowezekana kuleta ushindani kwa sababu kimesheheni majina makubwa ambayo hayana budi kupambana na kujijenga ili kuweza kuhakikisha wanakaa nafasi nzuri na ya pekee kuwa na matokeo mazuri yanayotakiwa klabuni hapo.

Utawala wa City kwa misimu miwili ulikuwa wa aina yake kiasi kwamba hakukuwa na klabu iliyokuwa na matazamio ya kunyanyua ubingwa mbele yao kutokana na aina ya soka walilokuwa wanalicheza. Msimu huu mambo yamewaendea kombo kabisa vijana hao wa Guardiola.

Huwa ni kawaida kwa mfumo unaosumbua kutafutiwa suluhisho na hilo ndilo lililoweza kutokea ndani ya kikosi cha Man City. Kwa sasa amekuwa akipoteza mechi za kawaida sana kutokana na mfumo wake kuwa mashuhuri sana na kila klabu imeweza kuuzoea na kuona wa kawaida sana tofauti na hapo awali.

Pamoja na kuwa na matokeo ambayo kwa hakika siyo mazuri sana kwa upande wake lakini anaamini kwamba bado ana uwezo wa kutetea ubingwa hata kama yupo alama 11 nyuma ya kinara wa ligi hiyo Liverpool ambaye ameweza kujizatiti hapo baada ya mechi zake 14 alizoweza kushiriki ndani ya ligi.

Tatizo kubwa linaloonekana kumsumbua kocha huyo ni safu yake ya ulinzi kuwa na mapungufu makubwa ambayo inaruhusu timu pinzani kupenya mara kwa mara. Jambo hilo ndilo linaloonekana kuwa na changamoto kubwa kikosini hapo. Imani ya kocha ni kutengeneza wale alionao ili kukidhi mahitaji ya kikosi chake.

Kinachoweza kuwa na changamoto kwake kuongeza wachezaji kwa sasa atalazimika kuuza kwanza wale alionao ili kuongeza sura mpya. Kama klabu wao hawajaonesha nia yoyote ya kuwaachia nyota wao kwa sasa ambao ni wakongwe kwa klabu yao. Bado wanafikiria juu ya kuwapunguza wengine ambao mikataba yao ipo ukingoni. Hivyo, kwa kipindi hiki watabaki na nyota hao hadi mwishoni mwa msimu huu.

2 Komentara

    Vzur tu

    Jibu

    Gud news

    Jibu

Acha ujumbe