Heshima Imerudi Huko Uingereza!

Baada ya miaka mingi ya kupuuzwa kwamba soka la Uingereza limeshuka na kupoteza hadhi yake sasa ni wakati wa kusema ile heshima ya soka la taifa hilo imerudi upya kwa kasi ya ajabu sana. Kama ilivyo siku zote soka ni mchezo wa wazi unaoonekana bila kificho chochote.

Hili linatokana na uhai wa kisoka uliooneshwa na klabu zinazoshiriki michuano mbalimbali mikubwa barani Ulaya ikiwemo ile ya klabu bingwa na ile ya Europa. Kuanzia kampeni nzima ya kufuzu katika michuano hiyo hadi hatua iliyobaki ya fainali mambo yamekuwa ya kipekee sana kwa ligi ya Uingereza.

Klabu zilizopata nafasi ya kuwakilisha ligi yao zimewakilisha vilivyo na kwa namna ya pekee kuweza kurejesha hadhi ya ligi yao. Baadhi ya klabu ambazo zinastahili heshima kubwa kwa kuweza kuleta mapinduzi ya pekee katika soka ni Manchester City, Manchester United, Arsenal, Chelsea, Tottenham na Liverpool ambazo zote ziliweza kuonesha upinzani na kujituma kwa aina yake ili kuhakikisha wanasalia kwenye michuano.

Hivi sasa ni wazi kusema kwamba kati ya makombe hayo makubwa mawili hakuna hata moja litakalotoka nje ya taifa hilo. Makombe yote yatachezwa nje ya taifa hilo lakini yatarudi ndani ya ardhi hiyo bila kupoteza radha halisi ya makombe yenyewe. Kwa hakika ni suala la kihistoria sana kwani ni miaka mingi jambo hilo lilipotokea.

Ni ama Liverpool au Tottenham katika UEFA lakini upande wa pili ni ama Chelsea au Arsenal kupata nafasi ya kunyanyua kombe. Katika hatua hiyo klabu zote hizi zina njaa ya aina yake kupata kombe hilo kutokana na kukosa kombe la aina hiyo kwa kipindi cha miaka mingi sana hadi sasa.

Chelsea na Arsenal watakutana kupigana vilivyo baada ya hapo jana kufuzu kwenye michuano hiyo na kufanikiwa kuziondoa timu pinzani ambazo nazo zilionesha upinzani wa aina yake kuhitaji kombe hilo muhimu kabisa. Klabu hizi za Uingereza zilionesha ukomavu kulihitaji zaidi kombe hilo.

Arsenal alikutana na Valencia ambao alifanikiwa kuwatoa kwenye michuano hiyo kwa matokeo ya 7-3 ikishuhudia Aubameyang akifanya maajabu ya aina yake ndani ya mchezo huo kwa kuwapa dozi nzito Valencia huku ikishuhudia soka safi sana kutoka kwa mshambuliaji mwenzake Lacazzete ambaye alifumania nyavu pia.

Huku Chelsea akikutana na Frankfurt alikutana na upinzani wa aina yake na kupelekea mechi yake kufika hadi dakika ya 120 huku kukiwa hakuna hata mmoja aliyemuondoa mwenzake kwa matokeo ya kawaida na kufanya uamuzi wa mafahari hao kuamriwa kwa mikwaju ya penati ambayo ndiyo imempeleka Chelsea hatua ya fainali.

Kufuzu kwa klabu hizo nne zinazotokea taifa moja kunatuvuta miaka ya 1990 ambako soka la Uingereza lilikuwa ni kioo cha pekee sana kabla ya utawala wa Hispania kupiku miaka ya 2000; kwa wakati huu tunaweza kusema tayari ramani nzima ya soka la Uingereza imerejea katika utawala wake wa miaka ya nyuma.

3 Komentara

    Noma sana.

    Jibu

    Gud

    Jibu

    Habari njema

    Jibu

Acha ujumbe