João Pedro amesema yuko tayari kubeba jukumu na matarajio ya kufunga mabao akiwa mshambuliaji namba tisa wa Chelsea.

Pedro alifunga mabao mawili wakati Chelsea walipomaliza maandalizi yao ya msimu kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Real Sociedad mwishoni mwa wiki.
Mabao hayo mawili yaliendeleza kiwango chake kizuri katika mechi za maandalizi ya msimu, ambapo Pedro amefunga mabao saba katika michezo ya majira haya ya kiangazi.
Pedro alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Msimu wa Chelsea 2025/26 baada ya kufunga mabao 23 katika msimu wake wa kwanza, na sasa yuko tayari tena kubeba jukumu la kuhakikisha timu inapata mabao.
Licha ya kuwepo kwa mjadala kuhusu nafasi yake bora zaidi uwanjani, Pedro amesema kwamba daima amekuwa mshambuliaji namba tisa.
“Nafasi yangu daima imekuwa namba tisa. Lakini kwa sababu nina uwezo mzuri wa kiufundi, ninaweza kushuka chini zaidi au kwenda pembeni. Ninachotaka ni kucheza na kuisaidia timu uwanjani.” Pedro aliiambia chelseafc.com.
“Wakati mwingine nitakuwa nyuma zaidi, na wakati mwingine nitakuwa ndani ya boksi. Kitu ambacho siwezi kupoteza ni ile silika ya kujua ninapaswa kuwa wapi uwanjani. Wakati mwingine kwenye mpira, unahitaji tu kuhisi.Ukiendelea kukaa ndani ya boksi pekee, huenda usipate nafasi nyingi. Lakini ukikaa nje ya boksi, unaweza kuwa mbali na lango. Kwa hiyo, ninahitaji kutumia hisia hiyo kisha nifunge mabao.”
“Nilipokuwa mdogo, nilicheza katika nafasi tofauti; nadhani hilo limenisaidia sana. Lakini tuna wachezaji bora katikati ya uwanja, hivyo nitazingatia zaidi kufunga mabao!”



