Kocha wa Italia, Luciano Spalletti, anakiri kuwa alikuwa na “uhusiano wa kutatanisha” na Rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, lakini atasalia kuwa “rafiki mkubwa” wa Francesco Totti.

Spalletti alizungumza kwa kifupi kuhusu maisha yake ya ukocha katika Roma na Napoli kupitia RAI 1, akijikita zaidi kwenye mahusiano yenye utata aliyowahi kuwa nayo.
“Hakuna jiji jingine lenye furaha na huzuni kama Naples. Nitaendelea kubeba furaha niliyoishuhudia huko,” Spalletti alisema kupitia Gazzetta.
Napoli walitwaa taji lao la kwanza la Serie A baada ya miaka 33 chini ya Spalletti msimu wa 2022-23, lakini kocha huyo aliachana na Stadio Maradona wiki chache tu baada ya kutwaa ubingwa huo wa kihistoria.
“Nilikuwa na uhusiano wa kutatanisha na De Laurentiis. Kwa kujitolea kwangu, ningependelea angeonyesha utu zaidi kwangu. Hatukuwahi kuzungumza tena tangu tulipoacha kufanya kazi pamoja.” Alikiri.



