Leon Goretzka alikuwa karibu kufikia makubaliano ya kujiunga na AC Milan akitokea Bayern Munich msimu huu wa joto, lakini sasa Rossoneri wamepunguza kasi na kutopendelea tena dili hilo. Wakati huohuo, Juventus pia bado hawana uhakika kufuatia kushindwa kwao kufuzu kucheza UEFA Champions League msimu ujao.

Leon Goretzka ni miongoni mwa wachezaji wakubwa ambao mikataba yao itaisha mwishoni mwa Juni. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 amekuwa Bavaria kwa misimu minane iliyopita, akishinda mataji saba ya ligi, vikombe vitatu vya Ujerumani na taji la UEFA Champions League 2019–20.
Kuelekea mwisho wa msimu wa 2025-26, ripoti kutoka Italia zilidai kwamba AC Milan walikuwa karibu kukamilisha dili la kumsajili Leon Goretzka, lakini mzozo mkubwa uliotokea San Siro katika wiki za mwisho za msimu unaonekana kusimamisha mpango huo.
AC Milan walishindwa kufuzu kucheza UEFA Champions League msimu ujao, wakikosa nafasi hiyo siku ya mwisho ya msimu licha ya kuwa walitumia muda mwingi wa mwaka wakiwa nafasi ya pili. Kutokana na hilo, klabu iliamua kuachana na kocha mkuu Massimiliano Allegri, mkurugenzi wa michezo Igli Tare, mkurugenzi wa kiufundi Geoffrey Moncada na CEO Giorgio Furlani, katika taarifa kali iliyotolewa siku moja baada ya msimu kumalizika.
Hali hiyo imeacha Rossoneri wakiwa na sintofahamu kubwa kuanzia ngazi ya uongozi hadi chini, na mkakati wao wa usajili bado haujawa wazi kutokana na kutokuwepo kwa kocha mkuu wala viongozi wa michezo na kiufundi.
Kwa mujibu wa La Gazzetta dello Sport, hali hii ya sintofahamu Milan inamaanisha kwamba Leon Goretzka sasa anapatikana tena kwa vilabu mbalimbali barani Ulaya.

Ripoti ya Jumatano inadai kwamba mawakala wa Leon Goretzka wameanza mazungumzo kuhusu uwezekano wa uhamisho wake na vilabu kadhaa “vikubwa” barani Ulaya, vikiwemo Arsenal FC, Chelsea FC na Juventus.
Juventus walikuwa tayari walikuwa wameanza kuomba taarifa kuhusu uwezekano wa kumpata Leon Goretzka mapema msimu, na hawakutishwa na madai ya mshahara wake unaoweza kuwa kati ya euro milioni 6 hadi 7 kwa mwaka.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa AC Milan, Juventus pia walishindwa kufuzu kucheza UEFA Champions League katika wiki za mwisho za msimu, na kwa sababu hiyo Bianconeri wanatajwa kuchukua muda kabla ya kutoa mikataba mikubwa, wakijua wanapaswa kutumia fedha kwa uangalifu bila kipato cha mashindano makubwa ya Ulaya.


