Vumbi la 2018/19 limeshatulia ndani ya ligi ya Uingereza sasa kilichobaki ni historia na nini kikatokea msimu ujao kwa klabu nyingine ambazo kwa hakika zimeonesha uwezo ambao hauendani na historia zao pia kwa zile ambazo makocha wao wanaamua kuyaanza maisha yao nje na pale walipokuwa.

Kuna baadhi ya walimu ambao kwa hakika wamefanya makubwa sana ndani ya ligi walizokuwemo hivyo kuuza sana sokoni kwa uwezo wao nao wanaweza kutimka kwenye klabu zao; pia, wengine ambao ligi hiyo imekuwa sio rafiki kwao wametimka katika klabu zao ili kupisha wengine.

Baadhi ya makocha hao ni:

Mauricio Pochettino (Tottenham), ni aina ya walimu ambao wanajua soka linataka kitu gani na klabu yake inataka wachezaji wa aina gani. Kwa hakika ameweza kuleta ushindani wa pekee sana ndani ya ligi hiyo ya Uingereza akiwa na historia ndani ya msimu huu zaidi ya kuuza wachezaji hajafanya usajili wowote mkubwa ili kujijenga lakini ametumia kikosi chake cha muda wote kupata matokeo na kupenya vikwazo vikubwa. Baadhi ya klabu zikiwemo Juventus, PSG na Bayern Munich zimeanza kumnyemelea tayari.

Maurizio Sarri (Chelsea), msimu wake ndani ya Chelsea ulianza kwa matunda mazuri sana lakini kadri ligi ilivyopamba moto alibadilika kabisa na kikosi chake kikaonekana kinaanza kupoteana sana lakini kama bosi wake atatokea kutokuridhishwa na jitihada zake za hapa mwisho wa ligi na pamoja na Chelsea kunyanyua kombe la Europa, kuna kila dalili ya kocha huyo kurejea kwao Italia ambako klabu ya Roma wanamhitaji.

Nuno Santo (Wolves), heshima kubwa anayopewa kocha huyu kwanza kabisa ni kuweza kuijenga timu yake kiushindani ndani ya ligi ya Uingereza. Akiwa na timu ambayo imepanda ligi ndani ya msimu mmoja pekee na kupata mafanikio ya kufika hadi nafasi ya saba ndani ya ligi ni jambo la mafanikio makubwa. Imekuwa ni kawaida kwake kuweza kuwaadabisha wakubwa kabisa kama Tottenham, Chelsea, Man Utd, na Arsenal. Hadi sasa anawindwa na klabu ya Chelsea kama itatokea wamemwagana na Sarri.

Rafa Benitez (Newcastle), chanzo kikubwa cha kutimka ni pamoja na mkataba wake kuwa tayari umefikia ukomo hivyo kama watakawia kumsainisha kandarasi nyingine anaweza kuwa safarini maana hata takwimu zake zinambeba sana yeye kusakwa na klabu nyingine. Kuna kila dalili ya yeye kutua Celtic ili kurithi mikoba ya Brendan Rodgers au akatua Roma.

ONI MOJA

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa