Mwisho wa wiki iliyopita michuano ya ligi ya Ujerumani, Bundesliga ilirejea tena uwanjani ikiwa imepita muda wa miezi miwli tangu isimamishwe. Ligi hiyo kubwa ya nchini Ujerumani ni moja ya ligi kubwa sana Ulaya na imekuwa ni ya kwanza kurejea tena tangu Corona isababishe majanga duniani.

Angalau sasa tunaona soka linarudi katika utamu wake tena. Angalia mambo ambayo binafsi nilijifunza baada ya ligi kurejea tena:

Mtazamo wa ugonjwa huu na soka ukoje?

Mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 umebadili kabisa sura ya soka na ukawaida wake. Kumekuwa na klabu pamoja na mamlaka mbalimbali nchini Ujerumani ambazo zimejaribu kuzuia wachezaji kupatwa na maambukizi ya ugonjwa huo. Kuna mpangilio wa utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa watu hawaambukizani tena.

Wikiendi hii, timu zilifika uwanjani kwa kutumia magari kadha wa kadha ili kuhakikisha watu wanakaa mbali mbali wawapo katika majukumu yao kisoka na kijamii kwa ujumla. Wachezaji wote walivaa masks wakati wakiingia uwanjani. Ile mechi kubwa ya Revierderby ilitawaliwa na utulivu wa aina yake katika dimba maarufu la klabu ya soka ya Borussia Dortmund, Signal Iduna Park. Wachezaji wa Dortmund walitoa heshima zao maarufu kwa Yellow Wall kana kwamba kulikuwa na mashabiki wao 25,000 mpaka mwisho wa mchezo pale kipyenga kilipopulizwa.

Mpangilio wa mambo yalikuwa sawia kabisa na yatakuwa hivyo mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo tena.

Haaland anaendeleza soka tamu

Wakati wachezaji wengi wa Bundesliga wakiwa bado wanahangaika na majanga yaliyotokea, mchezaji anayefunga mabao kadri anavyotaka kutoka klabu ya soka ya Dortmund ambaye ni mshambuliaji, Erling Haaland bado aliendeleza kabumbu safi kabisa alipokuwa dimbani. Mchezaji huyo kutoka Norway alifunga bao lake la kumi katika ligi ya Bundesliga akiwa ameshiriki mechi tisa pekee.

Ilimchukua muda wa dakika 28 kwa mshambuliaji huyo kupata bao lake hilo akiisaidia klabu yake ya Dortmund kuondoka na alama tatu kwa matokeo ya 4-0 dhidi ya mahasimu wao Schalke 04. Ikijumlishwa magoli yake aliyofunga kule Salzburg, kwa sasa Haaland amepachika jumla ya mabao 41 ambayo ni bora sana katika mashindano yote msimu huu.

Mafanikio zaidi kwa Robert Lewandowski

Mchezaji Haaland hakuwa yeye pekee ambaye alirudi katika amsha amsha yake ya mwanzo kutoka ile ya kipindi cha kabla ya miezi miwili iliyopita. Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Bayern Munich, Robert Lewandowski alipachika bao lake la 26 kwa msimu huu na kuisaidia timu yake kushinda 2-0. Kwa kufanya hivyo akawa amefikisha jumla ya mabao 40 katika mashindano yote kwa msimu huu.

Huyu ni mshindi mara nne wa tuzo ya Bundesliga Golden Boot. Alikuwa ni mchezaji wa tatu kuweza kufikia kilele cha jumla ya mabao 40 kwa misimu mitano mfululizo. Kwa kuweza kufikia kiwango hicho kwa sasa tayari anaungana na wachezaji wakali duniani, Lionel Messi pamoja na Cristiano Ronaldo.

Msala kwa RB Leipzig

Mambo yangekuwa poa sana kwa klabu ya soka ya RB Leipzig wikiendi hii endapo goli la mchezaji Robin Koch kwa klabu ya soka ya Freiburg lisingekataliwa. Hata hivyo, walijitutumua sana kuweza kupata sare ya 1-1. Kwa kweli mbio zao za kuwania taji kwa sasa zimeshayumba. Kwa sasa wana alama saba nyuma ya wanaoongoza ligi, Bayern na wanakalia nafasi ya nne ingawa walikuwa vizuri sana katika nusu ya kwanza ya msimu huu. Ubora wao haukuwa ukiridhisha sana. Hawakuwa kama ni timu ambayo iliikimbiza moja ya klabu kubwa za Uingereza, Tottenham Hotspur sehemu ile ile na dimba lile lile mwezi wa tatu mwaka huu.

Kuyumba kwa Frankfurt

Eintracht Frankfurt walipokea kipigo chao ikiwa ni kwa mara ya nne sasa mfululizo kwenye Bundesliga. Frankfurt wameshindwa kujiweka vyema zaidi katika kampeni zao za mwaka huu ukilinganisha na zile za mwaka jana ambapo walifanikiwa kufikia hatua ya nusu fainali ya michuano mikubwa ya Europa League barani Ulaya. Hata hivyo upande wa Adi Hutter ulishindwa kwa sababu uliwapoteza washambuliaji wake tegemezi, Luka Jovic pamoja na mwenzake Sebastien Haller.

Wale waliochukua nafasi zao, Andre Silva pamoja na Bas Dost hawakuweza kufanya lolote kufunga magoli katika mechi yao muhimu. Kwa sasa bado wana kiporo cha gemu moja na wanakalia nafasi ya 13 ya msimamo wa ligi hiyo, wana alama tano nyuma ya wale wanaokaribia kushuka daraja na huenda mambo yakawa mabaya endapo wasipokuwa makini kwa sababu wanakutana na Bayern kesho Jumamosi.

51 MAONI

  1. Wote tumejifunza vitu vingi sana ikiwepo na jinsi ya kujikinga dhidi ya huu ugomjwa wa corona ,pia ni matumaini yangu tunaendelea kujikinga .Asante mwandishi wa makala kwa taarifa nzuri.

  2. Ila tripu hii naimani watafanya vzr mno.na kuhusu kujikinga bila shaka hawatakiuka masharti watazingatia sheria inavyosema kwa ajili ya afya zao na watu watakao wazunguka

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa