Klabu ya Manchester United imeendeleza ubabe wake wa kushinda baada ya leo kupata ushindi wake wa tisa mfululizo kwenye Manchester derby dhidi ya Manchester City.
Klabu ya Manchester United imefanikiwa kuwafunga mahasimu zao mabao mawili kwa moja katika mchezo uliokua na ushindani mkubwa sana na wa kusisimua. Mchezo huo umeifanya Man United kua nyuma kwa alama moja dhidi ya klabu ya Manchester City.
Mchezo huo ulioanza kw kasi huku Manchester City wakimiliki mchezo kipindi cha kwanza lakini ni Man United waliofanikiwa kutengeneza nafasi za hatari katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo ambacho kilimalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Kipindi cha pili kilikua kipindi cha kila timu kutafuta alama tatu muhimu katika mchezo huo wa derby wenye msisimko mkubwa, Kocha Pep Guardiola alifanya mabadiliko na kumuingiza Jack Grealish akitoka Phil Foden na mabadiliko hayo yalimlipa baada ya Jack Grealish kuifungia klabu hiyo bao la kuongoza dakika ya 60 ya mchezo.
Klabu ya Manchester United baada ya kufungwa haikukata tamaa na yenyewe ikaanza kutafuta nafasi ya kusawazisha bao ambalo wametanguliwa na mahasimu wao, Wakati huo Manchester City wakiendelea kumiliki mchezo dakika ya 78 Bruno Fernandes anamalizia pasi nzuri ya Carlos Casemiro na kuisawazishia klabu hiyo goli na matokeo kua moja kwa moja.
Manchester United hawakuishia hapo dakika tatu mbele kwa maana ya dakika ya 82 ya mchezo klabu hiyo ilifanikiwa kupata bao la pili na la mwisho kwenye mchezo huo kupitia kwa Marcus Rashford na kuifanya klabu hiyo kutoka nyuma na kupindua meza kibabe kwenye derby ya Manchester. Man United imefanikiwa kusogea hadi nafasi tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 38 kwenye michezo 18 waliyocheza mpaka sasa.


