Michael Carrick ameazimia kumbakiza Mason Mount katika kikosi cha Manchester United msimu huu wa kiangazi, licha ya klabu hiyo kupokea maulizo kadhaa kutoka ndani na nje ya Uingereza kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo huyo, kwa mujibu wa TEAMtalk.

Kipaumbele kikubwa cha Manchester United katika dirisha hili la usajili ni kuimarisha safu ya kiungo, huku ikikaribia kukamilisha usajili wa Andrey Santos kutoka Chelsea.
Ederson wa Atalanta pia alikuwa akitarajiwa kujiunga na Old Trafford, lakini matatizo yaliyojitokeza kwenye vipimo vyake vya afya yameifanya hatma ya usajili huo kubaki mashakani.
Mount mwenye umri wa miaka 27 amekuwa akikumbwa na majeraha tangu alipojiunga na Manchester United akitokea Chelsea mwaka 2023.
Hata hivyo, msimu uliopita alianza mechi 12 za EPL, ikiwa ni mara ya kwanza kufikisha idadi hiyo ya mechi za kuanza tangu ajiunge na klabu hiyo miaka mitatu iliyopita.
Licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara, Manchester United haiko tayari kujadili uuzaji wake, ingawa kuna vilabu vya Uingereza na nje ya nchi vinavyomfuatilia.



