Mikel Arteta ameendelea kujifunga na Arsenal kwa kukubaliana mkataba mpya na mabingwa hao wa EPL.

Kuongezwa kwa mkataba wa Arteta wa kuwa kocha mkuu wa Arsenal ambao ulikuwa unatarajiwa kufikia mwisho wa msimu kulionekana kuwa jambo la kawaida.
Na Press Association inaelewa kwamba masharti ya mkataba mpya sasa yamefikiwa. Hata hivyo, haitarajiwi kwamba taarifa rasmi ya kuendelea kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 itatangazwa hivi karibuni.
Arteta alianza kuinoa Arsenal mwaka 2019 na ameiongoza klabu hiyo kurejea kwenye kilele cha soka la England, huku Gunners msimu uliopita wakitwaa taji lao la kwanza la ligi baada ya miaka 22.
Kikosi cha Arteta kilikuwa kimeanza utetezi wa taji lao kwa rekodi nzuri ya ushindi katika kila mchezo, hadi walipopata kipigo cha kushtukiza cha 3-0 dhidi ya Brighton kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Alipoulizwa kuhusu mkataba wake mpya kabla ya mchezo dhidi ya Seagulls, Arteta alisema: “Nafikiri sote tunaelewana kikamilifu; muda sahihi utakapofika, tutakamilisha hilo. Hakuna jambo la kuwa na wasiwasi nalo.”
Mbali na kumaliza kusubiri kwa Arsenal kutwaa taji la ligi, Arteta pia aliiongoza Arsenal kufika fainali ya kwanza ya Champions League baada ya miaka 20.

Arsenal walifungwa na Paris Saint-Germain kwa penalti, lakini katika siku chache kuelekea fainali hiyo iliyochezwa Budapest, mmiliki mwenza wa Arsenal, Josh Kroenke, alisema: “Kumuweka Mikel hapa ni kipaumbele cha juu kabisa, na nafikiri habari njema kwa mashabiki wa Arsenal duniani kote ni kwamba anafurahia mradi huu, anafurahia kuwa hapa na tangu kipindi chake akiwa mchezaji hadi sasa, yeye ni mtu wa Arsenal kwa kila hali.”
Baada ya kipigo chao cha kushtukiza kwenye Uwanja wa Amex siku ya Jumamosi, Arsenal watarudi kwenye mechi za ushindani kwa kucheza nyumbani dhidi ya Leeds Oktoba 10.


