Kulikuwa na hisia kwamba kuondoka kwa Mohamed Salah kutoka Liverpool kungekuwa jambo lisilo la kawaida, lakini wachache walitarajia angeelekea katika klabu anayotarajiwa kujiunga nayo sasa.

Baada ya miezi kadhaa ya tetesi kufuatia kuondoka kwake mwishoni mwa msimu uliopita, gwiji huyo wa Misri anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu ya Trabzonspor inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki (Super Lig), kwa uhamisho wa bure. Hatua hiyo itaweka mwisho wa safari ya mmoja wa wachezaji waliotengeneza historia kubwa zaidi katika enzi za kisasa za Ligi Kuu Uingereza.
Kwa mashabiki wa Liverpool, kumuona Salah akiwa amevaa jezi ya rangi ya maroon na buluu ya Trabzonspor kutahitaji muda kuizoea, kutokana na hadhi kubwa aliyojijengea akiwa Anfield.
Kwa kipindi cha miaka tisa, Mohamed Salah alikuwa moyo wa mafanikio ya enzi ya dhahabu ya kisasa ya Liverpool chini ya Jurgen Klopp, akiwa chanzo cha mara kwa mara cha ushindi kupitia kiwango chake cha kipekee. Hata hivyo, baada ya msimu wake wa mwisho kuwa na changamoto nyingi akiwa Merseyside, safari ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34 sasa inaendelea katika klabu ya Trabzonspor.
Klabu ya Trabzonspor, ambayo kwa kawaida hutajwa kama nguvu ya nne kubwa nchini Uturuki nyuma ya vigogo wa Istanbul Galatasaray, Fenerbahce na Besiktas haikuficha furaha yake Jumanne jioni.

Trabzonspor walithibitisha rasmi hatua hiyo kupitia taarifa fupi kwenye akaunti yao ya X, wakisema: “Mazungumzo yameanza kuhusu uhamisho wa mchezaji wa kulipwa Mohamed Salah kujiunga na klabu yetu.”
Kufikia usiku wa Jumanne, klabu hiyo ya Uturuki ilitoa pia ratiba kamili ya safari ya Salah, ikithibitisha ni lini anatarajiwa kuwasili ili kufanyiwa vipimo vya afya na kukamilisha rasmi mkataba wake wa miaka miwili.
Uhamisho wa Mohamed Salah kwenda Trabzonspor unakuja baada ya miezi kadhaa ya tetesi zilizomhusisha na klabu mbalimbali duniani.
Baada ya kuwa mchezaji huru, klabu kadhaa za Saudi Pro League, zikiwemo Al-Ittihad, Al-Hilal, Al-Nassr, Al-Ahli, Al-Qadsiah na Al-Diriyah, zilikuwa zikifuatilia kwa karibu hali yake. Hata hivyo, Salah aliamua kuendelea kucheza soka barani Ulaya, jambo lililomshawishi zaidi kuliko kuhamia Saudi Arabia.
Mapema katika dirisha la usajili, Salah alikuwa kwenye mazungumzo ya hatua za mwisho na Besiktas, lakini mazungumzo hayo yalikwama. Mkurugenzi wa soka wa Besiktas, Onder Ozen, alieleza kuwa mazungumzo yalivunjika kutokana na tofauti kuhusu muundo wa kifedha wa mkataba pamoja na haki za matumizi ya taswira (image rights).
Baada ya Besiktas kujiondoa kwenye mazungumzo, Trabzonspor, waliomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya Uturuki msimu uliopita na ambao wanajiandaa kushiriki hatua za mchujo za Europa League, walichukua hatua haraka na kufanikisha makubaliano.

Akiwa Trabzonspor, Salah atakutana tena na sura aliyoizoea kutoka Ligi Kuu Uingereza, kipa wa zamani wa Manchester United, Andre Onana, ambaye amerejea klabuni hapo kwa mkopo kwa mara ya pili.
Kuondoka kwa Salah kutoka Anfield kulichochewa na msimu mgumu wa 2025/26. Baada ya kusaini nyongeza ya mkataba wa miaka miwili kabla ya msimu wa 2024/25, mshambuliaji huyo aliondoka kabla ya mkataba huo kumalizika.
Kwa mujibu wa talkSPORT, Salah alikubali kurekebisha mwaka wa mwisho wa mkataba wake uliokuwa na thamani ya pauni milioni 20 kwa mwaka, ili aruhusiwe kuondoka kwa uhamisho wa bure. Mfumo huo wa makubaliano unafanana na ule uliotumika wakati wa kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, mwaka 2024. Inadaiwa pia kuwa mazungumzo ya kuvunja mkataba kwa maelewano yalianza kabla ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwishoni mwa mwezi Desemba.
Uwanjani, kiwango cha Salah kilishuka ukilinganisha na misimu yake ya awali. Msimu uliopita alifunga mabao saba na kutoa asisti saba katika mechi 27 za Ligi Kuu Uingereza. Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya kuachwa benchi katika baadhi ya mechi muhimu za Ligi ya Mabingwa Ulaya, jambo lililosababisha mvutano wa wazi kati yake na kocha Arne Slot, hali iliyotafsiriwa kuwa mwanzo wa mwisho wa safari yake ndani ya Liverpool.
Licha ya kuwa na msimu wa mwisho uliokuwa na changamoto katika ngazi ya klabu, Mohamed Salah alionyesha kuwa ubora wake bado upo alipoiwakilisha Misri katika Kombe la Dunia majira ya kiangazi yaliyopita. Akiwa nahodha wa timu hiyo, aliiongoza kufika hatua ya 16 Bora kwa mara ya kwanza katika historia yake, akifunga bao moja na kutoa asisti mbili katika mechi tano alizocheza.



