Furaha ya mchezaji ni kuisaidia timu yake kupata matokeo kupitia yeye kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho wake. Jambo hilo huendana na kucheza mechi husika kwa juhudi zake na maarifa yake yote. Inapotokea mchezaji huyo anatoka na kwa upande mwingine inaonekana kama yeye ndiye tegemezi kwenye kikosi husika huibua hisia za tofauti.

Kuna msemo usemao uwepo wa baadhi ya wachezaji kwenye kikosi fulani huchochea matokeo kupatikana hata kama timu hiyo inacheza soka ambalo halina mvuto wa namna yake. Jambo hilo kwa upande mwingine huwa na uhalisia kutokana na heshima na wanavyochukuliwa wachezaji hao wakiwa uwanjani.

Wachezaji kama Ronaldo, Messi, Hazard, Mbappe wakikosekana katika timu zao hufanya timu pinzani kucheza soka la kujiachia sana na hatimaye hata kuondoka na ushindi kwenye mechi zao hizo. Suala hilo mara kadhaa huchangia kwa kiasi kikubwa kubadilika kwa mfumo wa kikosi hasa ule uliozoeleka siku zote.

Habari za Cristiano Ronaldo kuumia katika michuano ya kujifua kuelekea EURO 2020 kuliibua sura mpya kwa timu ya taifa ya Ureno na klabu yake ya Juventus huku wakiwa wanafikiria namna ya kupata alama ili waweze kupanda kwenye kundi lao kutokana na kuwa na matokeo mabovu ambayo yataigharimu timu yao.

Ni Ajali Ndogo Tu

Nyota huyo alitolewa uwanjani dakika ya 31 ya mchezo baada ya kushindwa kuendelea na mchezo ikiwa ni wakati aliokuwa akifukuzia mpira na kujikuta misuli inamzuia ashindwe kusonga mbele na kuamua kumfanyia mabadiliko ili kuzuia tatizo hilo lisizidi kuwa kubwa baada ya kupata majeraha hayo.

Baada ya mchezo nyota huyo alipofanyiwa uchunguzi na madaktari ilidhihirika kwamba hakupata tatizo kubwa sana kitu ambacho kilileta faraja kwa mashabiki zake na kwamba pamoja na majeraha hayo ataweza kurejea viwanjani baada ya wiki moja au mbili mara baada ya kutibiwa na klabu yake ikathibitisha kwamba atakuwepo uwanjani wakati wa mechi dhidi ya Ajax kwenye michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Baada ya kutoka mshambuliaji huyo timu yake iliendeleza soka safi lakini wakakosa kabisa nafasi ya kuliona lango la mpinzani wake na kufanya mechi hiyo kuisha kwa sare ya 1-1 na ni jambo ambalo wengi wameona kwamba wachezaji walikosa umakini ambao kwa kipindi Ronaldo yupo mchezoni ulikuwepo kwa asilimia kubwa.

Ni matumaini ya kila mmoja kwamba kikosi hicho kitarejea kama ilivyokuwa hapo awali na umakini wa aina yake maana kwa hali ilivyo ni kwamba umri wa Ronaldo umesonga na hawezi kuwa mchezaji tegemezi mara kwa mara kutokana na umri alionao. Hivyo, kama timu hawana budi kuwekeza kwa kumuandaa mtu ambaye atakuwa mbadala wake.

ONI MOJA

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa