Wapinzani wa Uingereza katika hatua ya robo fainali, Norway, wamezua mjadala baada ya kuhama kutoka hoteli yao ya timu iliyokuwa ikigharimu dola 250 kwa usiku huko Miami, siku moja tu baada ya kuwasili, kutokana na kutoridhishwa na mazingira na huduma zilizokuwepo.

Inadaiwa kuwa Erling Haaland pamoja na wenzake hawakuridhishwa na kelele za ujenzi zilizokuwa karibu na hoteli, ukosefu wa chumba maalumu cha mikutano, pamoja na umbali wa takribani kilomita nne kutoka hotelini hadi ufukweni.
Licha ya hoteli hiyo kuwa na bwawa la kuogelea la kifahari linalotoa mwonekano wa mandhari ya majengo marefu ya jiji, vyumba vikubwa vya hadhi ya juu vyenye mandhari ya kuvutia ya Florida, pamoja na huduma za kisasa zilizokidhi viwango vya juu, kikosi hicho kiliamua kuhama.
Kocha na wachezaji wa Norway wamezungumzia hadharani kutoridhishwa kwao na Hoteli ya The Dalmar iliyopo Fort Lauderdale, walikokuwa wamefikia awali, kabla ya kuhamia kwa haraka katika Hoteli ya Four Seasons iliyopo ufukweni kwa msaada wa watu wa kujitolea.
“Nadhani kulikuwa na mambo kadhaa ambayo yangeweza kuwa bora zaidi, na tukayarekebisha. Lengo lilikuwa kuboresha mazingira yetu na kujiandaa kwa kiwango bora kabisa kuelekea mchezo muhimu,”alisema nahodha wa Norway na nyota wa Arsenal, Martin Ødegaard.

Kocha wa Norway, Ståle Solbakken, aliongeza: “Kulikuwa na mambo machache ambayo hayakuwa sawa pale. FIFA ilikubaliana nasi kuhusu hilo na ilikuwa tayari sana kutusaidia.”
“Unahitaji kuwa na sehemu ya kukusanyika na kufanya mikutano ya timu. Kwa ujumla kulikuwa na mambo mengi madogo yaliyokuwa hayajakaa vizuri. Si kwamba hoteli hiyo haikufaa kuishi, lakini sisi tunahitaji kuwa pamoja kama timu, kuwa kitu kimoja na kudumisha umoja wetu.”
Kwa mujibu wa gazeti la Dagbladet, wachezaji kadhaa wa Norway walikatishwa tamaa na kiwango cha usafi katika Hoteli ya The Dalmar.
Wakati huohuo, VG iliripoti kuwa hoteli hiyo ilikuwa karibu na barabara yenye shughuli nyingi za magari, jambo lililoongeza usumbufu kwa kikosi hicho. Waandishi wa VG walijaribu kuzungumza na uongozi wa hoteli hiyo, lakini hawakuruhusiwa kutoa maoni.
Hali hiyo haikuwa maandalizi bora kwa taifa hilo la Scandinavia, ambalo linajiandaa kucheza robo fainali ya Taji la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Meneja wa msafara wa Norway, Truls Daehli, alisema: “Kulikuwa na mambo kadhaa katika sehemu tuliyokuwa tunakaa ambayo tulitamani yawe tofauti. Tuliona ilikuwa muhimu kuchukua hatua. Ni kana kwamba tutakuwa hapa kwa wiki moja zaidi, lakini tayari tumeshamaliza wiki sita nchini Marekani na sasa tunakwenda kucheza mchezo mkubwa zaidi katika historia ya kizazi hiki cha timu yetu.”



