Pep Guardiola na Manchester City ni moja ya klabu kuu zinazomwania beki wa pembeni wa AS Roma, Wesley França, huku wakipanga “maboresho ya muda mrefu” katika nafasi ya beki wa kulia, kwa mujibu wa Caught Offside.

Roma wanaaminika kukabiliwa na vita kubwa ya kumbakiza Wesley. Mchezaji huyo mwenye miaka 22, ambaye amefunga mabao matano na kutoa assists mbili katika mashindano yote msimu huu, anaripotiwa kuwaniwa na klabu kubwa kama Manchester City, FC Barcelona na Real Madrid.
Hizo ni baadhi tu ya klabu kubwa zinazomfuatilia, huku timu nyingine kadhaa za EPL pia zikitajwa kuwania huduma zake. Newcastle United nao wanadaiwa kuvutiwa naye, wakati Arsenal na Tottenham Hotspur pia wanahusishwa naye.
Hata hivyo, ni nia ya City ambayo inaweza kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kuhusu mustakabali wa Wesley, kwani ripoti hiyo inaeleza kuwa Pep Guardiola anapenda mabeki wenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali. Mbrazil huyo anaonekana kufaa mfumo huo kutokana na uwezo wake wa kucheza kama beki wa kulia au hata mbele zaidi pembeni katika pande zote mbili za uwanja.
Mfano wa mabeki ambao Guardiola amewatumia katika nafasi tofauti tofauti akiwa City ni Joao Cancelo, Rico Lewis, Josko Gvardiol na John Stones.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Wesley França angekuwa sehemu muhimu ya mpango wa “maboresho ya muda mrefu” katika nafasi ya beki wa pembeni kwa Manchester City. City walimruhusu Kyle Walker kuondoka majira ya kiangazi na mara nyingi wamemtumia Matheus Nunes katika nafasi hiyo msimu huu, licha ya kiungo huyo wa zamani wa Wolverhampton Wanderers kuwa kiungo zaidi kuliko beki.

Kutokana na Wesley kuwa na mkataba mjini Rome hadi mwaka 2030, baada ya kusaini kutoka klabu ya Brazil ya Flamengo majira ya kiangazi yaliyopita, AS Roma wako kwenye nafasi nzuri ya kujadiliana, na hivyo inaaminika kuwa dili lolote litahitaji “ofa kubwa.”
Lakini kama kuna timu inayoweza kutoa fedha nyingi kusajili beki nyota, basi ni Manchester City. Kati ya usajili wao 10 wa gharama kubwa zaidi katika historia, wanne wamekuwa mabeki.
Usajili wa gharama kubwa zaidi ulikuwa wa Joško Gvardiol aliyegharimu pauni milioni 77.6, huku hata beki aliyekuwa wa nne kwa gharama kubwa zaidi kwa City, Aymeric Laporte, akigharimu pauni milioni 57 mwaka 2018.
Wakati huo, nyota huyo wa Hispania alikuwa beki ghali zaidi katika historia ya City, lakini rekodi hiyo ilivunjwa walipomsajili João Cancelo, kisha tena walipompata Rúben Dias, na hivi karibuni zaidi wakati Gvardiol alipojiunga.
Hilo linaonyesha jambo moja wazi: kama City watataka kumsajili Wesley, kuna uwezekano mkubwa watafanikiwa kumpata.


