Shujaa wa Liverpool, Sadio Mané, ameanza kazi mpya isiyo ya kawaida kwa kuanzisha biashara ya maembe katika nchi yake ya Senegal. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 alijiunga na The Reds akitokea Southampton mwaka 2016 kwa ada ya pauni milioni 34.

Alikuwa sehemu muhimu ya safu hatari ya ushambuliaji pamoja na Mohamed Salah na Roberto Firmino, ambayo ilitumiwa na kocha wa zamani Jurgen Klopp kwa mafanikio makubwa.
Mané aliondoka Liverpool na kujiunga na Bayern Munich mwaka 2022 kwa ada ya pauni milioni 35, na kwa sasa anacheza katika klabu ya Saudi Arabia, Al-Nassr.
Inasemekana Mané amewekeza kiasi kikubwa cha pauni milioni 15 katika mradi unaoitwa SM10 Agro. Mradi huo unalenga zaidi kunufaisha mji wake wa Bambali, kijiji kilichopo umbali wa takribani maili 250 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Dakar.
Biashara ya nyota huyo wa Senegal inatarajiwa kuunda ajira 1,000. Katika mipango yake, Mané atahakikisha kunajengwa mashamba ya maembe, viwanda vya kusindika mazao pamoja na chuo cha kilimo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi Jumamosi, Septemba 19, Mané alisema: “Eneo la Sedhiou hupoteza kati ya asilimia 30 hadi 40 ya maembe linayozalisha kutokana na kushindwa kuyahifadhi na kuyasindika ipasavyo. Nataka utajiri unaotokana na ardhi yetu ubaki hapa hapa Senegal. Mpango huu utaajiri watu 1,000 tangu mwanzo.”

“Viwanda vya kusindika mazao vitajengwa Bambali, na kimojawapo kitajikita katika uzalishaji wa siagi ya maembe. Pia kutakuwa na shamba la maembe lenye ukubwa wa hekta 500, pamoja na kuanzishwa kwa chuo cha kilimo.
“Natamani vijana na wanawake wa eneo langu wapate fursa halisi za elimu. Huduma za usafirishaji na utoaji wa bidhaa kwa ajili ya SM10 Agro pia zitasaidia kuunda ajira zaidi kwa njia isiyo ya moja kwa moja.”
Naibu mkurugenzi wa SM10 Agro, Aminata Tope, aliongeza: “Tutatengeneza miti ya maembe 78,000, huku mavuno ya kwanza yakitarajiwa baada ya miaka mitatu. Chuo hicho pia kitakuwa na kituo cha utafiti na maendeleo, na kiwanda kitaweza kuzalisha tani 10,500 kwa mwaka.”
Uhisani wa Mané katika nchi yake ya Senegal ni jambo ambalo limekuwa likitajwa sana. Wakati janga la Covid-19 lilipoikumba dunia mwezi Machi 2020, winga huyo alitoa pauni 41,000 kwa Kamati ya Kitaifa ya Senegal iliyokuwa ikipambana na virusi hivyo. Pia alijenga hospitali ya umma yenye thamani ya pauni 455,000, ambayo inajumuisha kitengo cha huduma za uzazi.
Nyota huyo wa zamani wa Red Bull Salzburg alitoa pauni 250,000 kwa ajili ya kujenga shule ya sekondari ya umma inayotoa elimu bure, pamoja na kutoa kompyuta mpakato. Pia amefadhili ujenzi wa kituo cha mafuta na ofisi ya posta huko Bambali.
Mané alitwaa mataji sita akiwa Liverpool, yakiwemo Premier League na Champions League. Baada ya kufunga mabao 120 katika mechi 269 alizoichezea Liverpool kwenye uwanja wa Anfield, aliondoka na kwenda kucheza Bundesliga, ambako mambo hayakwenda kama alivyotarajia.

Baada ya kushindwa kuonyesha kiwango chake bora nchini Ujerumani, alijiunga na Al-Nassr mwaka mmoja baadaye, ambako bado anacheza hadi leo. Akielezea sababu iliyomfanya kuondoka Liverpool, alisema mnamo Novemba 2025:
“Liverpool ilikuwa kama nyumbani kwangu. Ilikuwa sehemu yangu ya faraja. Nikasema tujaribu kitu kingine kwa sababu nilikuwa karibu kushinda kila kitu hapa. Kwa hiyo changamoto yangu haikuwa kwa sababu ya… bila shaka baadhi ya mambo yanaweza kutokea au blah blah, lakini kwangu mimi hilo halikuwa jambo muhimu sana.”
“Motisha yangu ilikuwa kwenda sehemu nyingine na kujaribu kuona… kuondoka katika eneo langu la faraja na kufanya kitu tofauti upande mwingine. Hiyo ndiyo sababu yangu ya kusema, ‘Sawa, tujaribu.


