Tetesi za Usajili

Bayern Munich hawaoni ugumu wowote kurudi sokoni kupambana na Manchester City juu ya nafasi yao ya kumsajili nyota wa klabu hiyo, Sane pamoja na kwamba nyota huyo kwa sasa ana majeraha yatakayomuweka nje kwa kipindi kirefu cha zaidi ya miezi saba. Hiyo ni biashara hatari sana japo inaonekana kutowatisha kabisa Munich ambao wameonesha nia yao ndefu zaidi hapo.

Neema inazidi kumuangukia mlinzi wa klabu ya Manchester United, Lindelof mbali na hapo awali kubezwa sana kwamba hangeweza kuwa sehemu nzuri sana kwa kikosi hicho. Klabu hiyo imempa mkataba ambao anatarajia kuusaini katika siku za usoni kukiwa na ongezeko la mshahara tofauti na ule aliokuwa akiupokea hapo awali.

Maisha ya Eriksen ndani ya klabu yake yapo katika kipindi cha matazamio na yanasubiri maamuzi ya nyota huyo endapo atakuwa tayari kusaini kandarasi ya kuendelea kuhudumu kikosini hapo mbali na klabu za Madrid na Juventus kuonesha nia ya kutaka kumsajili. Spurs wataweka mazungumzo kuona kama nyota huyo ambaye anamezewa mate na kuwa ghali zaidi endapo atauzwa ili kuweka mambo sawa kabla ya dirisha la usajili kufungwa huko Ulaya.

Matuidi anaonekana kuanza kunyooshewa vidole na klabu ya Monaco ambayo inaamini kama itampata kiungo huyo basi itaweza kupiga hatua ndefu sana kutokana na uwezo wa nyota huyo. Klabu hiyo kwa wakati huu inauhitaji wa nyota kama hao ili kuweza kujijenga na kuonesha ushindani kwenye klabu yao kwa manufaa ya baadaye.

Nyota wa Manchester United na raia wa Chile, Alexis Sanchez hana mpango wa kuondoka ndani ya klabu hiyo mbali na kauli za kocha wa klabu hiyo kwamba hawezi kumtumia ndani ya kikosi chake cha kwanza hata kama ataendelea kusalia katika viunga vya timu hiyo. Klabu za AC Milan na Napoli zilionesha nia ya kumhitaji nyota huyo japo yeye hajaonesha nia yoyote ya kuihama klabu hiyo na kuonesha kwamba bado ataendelea kusalia hapo.

Mshambuliaji mtukutu raia wa Italia, Mario Balotelli anaonekana kupiga chini ofa ya kujiunga na klabu ya Flamengo na ameshawishika kwa nafasi kubwa sana kujiunga na klabu ya Brescia ambayo imeonesha nia ya kumpa mkataba mnono wa miaka mitatu jambo ambalo ameonekana kuvutiwa nalo. Klabu ya Flamengo inaonesha kwamba haijatishika na taarifa hizo na ina matumaini makubwa ya kumshawishi kujiunga nao.

Acha ujumbe