Siku moja pekee imesalia kabla ya Fountain Gate FC kuwa wenyeji wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, kwenye vita ya kuwania alama tatu kwenye mchezo utakaochezwa kesho Juni 18 kwenye Uwanja wa Shekh Amri Abeid Kaluta.

Yanga walipaa kwa ndege jana asubuhi kwenda Arusha na jana hiyo hiyo wakapata nafasi ya kufanya mazoezi ya kwanza wakiwa jijini humo.
Na ripoto ya Afisa Habari wa Yanga Ali Kamwe alisema: “Tunamshukuru Mungu kuwa kila kitu kipo sawa hapa Arusha, siyo mchezo mwingine rahisi, lakini tumekuja na dhamira ya kushindana na kushinda mchezo huu.”
Kikosi hicho kiliondoka kikiwa katika hali nzuri ya kujiamini baada ya kuendelea kufanya vizuri kwenye mbio za ubingwa, huku benchi la ufundi likisisitiza umuhimu wa kushinda mechi zote zilizosalia ili kutimiza malengo ya msimu huu.
Wachezaji wa Yanga walionekana wenye furaha na morali ya juu walipokuwa wakijiandaa na safari hiyo, ishara ya utayari wao wa kukabiliana na changamoto ya mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.
Wananchi wanaingia katika pambano hilo wakilenga kuendeleza matokeo yao mazuri ya msimu huu pamoja na kuimarisha nafasi yao kileleni mwa msimamo wa ligi, wakati mbio za ubingwa zikizidi kupamba moto kuelekea tamati ya msimu.



