Waingereza Wamtamani Samatta

Kuna taarifa zinaendelea kugonga vichwa vya habari kwamba klabu za Uingereza tayari zimeanza kuvutiwa na nyota wa Kitanzania, Mbwana Samatta anayekipiga katika klabu ya KRC Genk kwa mafanikio makubwa sana na uwezo wake mkubwa wa kuparamia nyavu anaozidi kuuonesha ndani ya ligi.

Japo sio klabu zenye takwimu za juu sana lakini ni jambo jema sana kwa mchezaji huyo kuanza kutambulika kiasi hicho nje ya mipaka na kuonekana ana nafasi kubwa sana ya kuweza kusonga mbele zaidi kwenye tasnia yake hiyo huku akiipeperusha vyema bendera ya Tanzania nje ya mipaka.

Nyota huyo mwenye miaka 26 amekuwa mwiba wa aina yake msimu huu akifunga magoli 32 na pasi za magoli sita kwenye michezo 52 ambayo ameweza kuingia uwanjani kuonesha uwezo wake mkubwa na wa pekee sana. Hayo ni mafanikio makubwa sana ndani ya mwaka mmoja pekee ndani ya klabu hiyo.

Mbali na hilo, pia ndiye anayeshikilia kitambaa cha unahodha ndani ya timu yake ya taifa jambo ambalo bado linampa nafasi ya kuendelea kung’aa zaidi kwenye upande huo wa soka. Na atashuhudiwa akiipeleka timu yake kwenye michuano ya AFCON mwaka huu baada ya kupata nafasi ya ushiriki.

Middlesbrough walikuwa wa kwanza kabisa kuanza kuonesha kumhitaji nyota huyo kutokana na uhitaji wao wa washambuliaji wa aina yake ambao kama klabu imewakosa kwa muda mrefu, na katika kuangalia zaidi sokoni wakakuta Samatta ni aina ya watu ambao wanaweza kutokomeza kabisa tatizo hilo.

Inaonekana tayari wapo kwenye mipango hiyo na hata kama kocha mpya ataweza kutua hapo kikosini baada ya Tony Pulis kushindwa kufikia malengo ya pale wanapotaka wao basi kwa hakika nyota huyo bado atakuwa kwenye mpango kazi wa klabu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa ambao unawavuta wengi.

Mfungaji wao wa muda wote kwa misimu miwili alikuwa ni Britt Assombalonga lakini anahitaji sana kupata mtu wa kusaidiana naye kutokana na kukosa muunganiko mzuri katika nafasi hiyo. Uwezo wake wa kufunga unaweza kuwa na tija ndani ya kikosi hicho kama akifanikiwa kwenye makubaliano japo klabu hiyo bado haishiriki ligi kuu lakini ni mwanzo mzuri sana.

2 Komentara

    Gud news

    Jibu

    Ni vizur aendele kukaza buti hatafika mbali

    Jibu

Acha ujumbe