Ili timu iweze kuwa imara huhitaji wachezaji bora na wenye weledi wa kuzuia timu yao isiweze kufungwa mara kwa mara. Uwepo wa wachezaji wa aina hii ni kiini cha kuwepo kwa kikosi bora kinachopambana kujenga historia fulani ndani ya klabu ambayo huwa na nia ya kufika mbali kihistoria na hata malengo mengine pia ya kutwaa vikombe.

Cafu, Javier Zanetti, Gianluca Zambrotta, Lilian Thuram ni miongoni mwa walinzi waliojenga historia kubwa sana kwenye soka na wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kile walichopaswa kukifanya kama wachezaji. Hawakuwa sehemu ya walinzi pekee na pia ndiyo walioanza kuonesha mapinduzi ya walinzi wanaopandisha mashambulizi kwenye timu zao.

Kuwa mlinzi wa upande wa kulia katika karne hii kunahitaji ubunifu, kasi na hata ujuzi uliotukuka kutokana na aina ya soka linalochezwa siku hizi. Kwa sababu huhitaji mtu anayepanda kushambulia bila kusahau majukumu yake ya kiulinzi ili kuifanya timu yake isielemewe pale inaposhambulia. Pia, huhitaji mtu mwenye uwezo wa kutengeneza pasi ya mwisho au kufunga.

Pamoja na kuona timu nyingi zikipigania kuwa na wachezaji wa aina hii, katika msimu huu pia kumekuwa na wachezaji wa aina yake hasa wenye uwezo wa kutengeneza mashambulizi na wakati huo huo kulinda. Baadhi ya wachezaji walioonesha uwezo huo kwa msimu huu kuwazidi wengine ni:

Matt Doherty (Ireland, Wolverhampton Wanderers), mlinzi huyo katika siku za usoni amekuwa msaada mkubwa sana kwenye kikosi cha timu yake ambacho kipo nafasi nzuri kwenye ligi kwa sasa pamoja na kuwa na ugeni kwenye ligi hiyo. Wamekuwa na wakati mzuri sana wa kujisifia kutokana na uimara wa nafasi hiyo.

Aaron Wan-Bissaka (England, Crystal Palace), katika umri wake wa miaka 21 anaonekana kufanya mambo ambayo ni makubwa sana na yenye heshima kubwa kabisa kwenye soka. Pamoja na mapungufu madogo yanayompelekea kupata kadi za njano na nyekundu akiwa uwanjani ambacho ni kitu kinachoonekana kumgharimu mara kwa mara pamoja na ubora wake huo.

Łukasz Piszczek (Poland, Borussia Dortmund), ameweza kuleta upekee katika kikosi cha Dortmund. Katika umri wake wa miaka 33 anaonekana kuwa imara zaidi kitu ambacho kimewasaidia Wajerumani hao kufikia hatua nzuri ndani ya ligi hiyo.

Trent Alexander-Arnold (England, Liverpool), ni mchezaji mwenye kasi na maamuzi ya haraka na bila shaka Liverpool wanafurahia sana kuwa na aina hii ya wachezaji kwenye kikosi chao kwa sababu anawapa kile wanachokihitaji kwa wakati sahihi.

Joshua Kimmich (Germany, Bayern Munich), amekuwa msaada sana katika ushindi ambao Bayern amekuwa akiupata uwanjani. Amechangia kwa kiwango kikubwa sana kupatikana kwa magoli mengi kwenye timu yake hiyo. Kwa umri wake kuna mazuri zaidi yatapatikana kutoka kwake kadri siku zinavyosonga.

3 MAONI

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa