Wesley Sneijder ameionya Arsenal kuwa wanaweza kufungwa kwa idadi kubwa ya mabao watakapokutana na mabingwa watetezi Paris Saint-Germain katika fainali ya UEFA Champions League.

Kiungo huyo wa zamani wa Inter Milan anaamini kuwa kama The Gunners hawatakuwa na nidhamu ya hali ya juu kabisa katika safu ya ulinzi, miamba hiyo ya Ufaransa ina uwezo mkubwa wa kushambulia na inaweza kurudia ushindi wao wa kikatili wa mabao 5-0 dhidi ya Nerazzurri msimu uliopita.
Arsenal wamefuzu kucheza fainali yao ya kwanza ya UEFA Champions League tangu mwaka 2006 baada ya ushindi mgumu wa nusu fainali dhidi ya Atlético Madrid.
Kikosi cha Mikel Arteta kwa sasa kinawania kufanya historia kwa kutwaa mataji mawili, huku ubingwa wa EPL pia ukiwa bado ndani ya uwezo wao. Hata hivyo, wanakabiliwa na mtihani mkubwa dhidi ya Paris Saint-Germain katika fainali ya Ulaya itakayochezwa Mei 30.
Kikosi cha Luis Enrique kilifika fainali baada ya ushindi wa jumla wa mabao 6-5 dhidi ya FC Bayern Munich, wakionyesha mchanganyiko wa soka la kuvutia la kushambulia pamoja na uimara wa kujilinda unaowafanya kuwa mabingwa watetezi wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa tena taji hilo.

Licha ya kukiri ubora wa mabeki wa kati wa Arsenal, kiungo wa zamani wa Inter Milan na timu ya taifa ya Uholanzi Wesley Sneijder alieleza wasiwasi wake kuhusu tofauti ya nguvu pembeni mwa uwanja wakati wa mahojiano na Hard Rock Bet.
Alisema: “Kama nikitakiwa kusema nani atashinda, ningesema Paris Saint-Germain. Lakini Arsenal hawafungwi mabao kirahisi. Wana safu imara sana ya ulinzi yenye mabeki wawili wa kati wa kiwango cha juu.”
“Siamini kama mabeki wao wa pembeni ni bora zaidi katika UEFA Champions League, na hapo ndipo PSG walipo na nguvu, hasa upande wa kushoto. Kila mwenye mapenzi na Arsenal ana matumaini kwamba Jurriën Timber atarejea na kuwa fiti kwa ajili ya fainali. Vinginevyo, itakuwa ngumu sana kwao. Lakini Arsenal pia wanajua namna ya kujilinda kwa kusaidiana, huku Declan Rice akishuka nyuma kusaidia safu ya ulinzi.”
Akizungumzia ushindi mkubwa wa mabao 5-0 wa Paris Saint-Germain dhidi ya Inter Milan mwaka jana, Wesley Sneijder alitoa mtazamo wake kuhusu namna fainali hiyo inaweza kuwa na matokeo makubwa.
Aliongeza: “Itakuwa mechi ya kuvutia. Nafikiri inaweza kufanana na fainali ya Inter Milan mwaka jana. Ninaamini inaweza kuwa [5-0]. Kabla ya mchezo ule niliona PSG wana faida, lakini Inter walikuwa na safu nzuri ya ulinzi na namna wanavyocheza mashambulizi ya kushtukiza.”

“Labda inaweza kuwa mshangao na Inter kushinda 1-0, lakini pia ingeweza kuwa usiku mgumu sana kwa Inter, na hiyo ndiyo hisia ninayo sasa [kwa Arsenal]. Inaweza kuwa mechi ngumu yenye Arsenal kushinda 1-0, na sisemi ‘ngumu’ kwa maana mbaya, kwa sababu kuizuia PSG kufunga ni jambo kubwa sana. Lakini hilo ni gumu kweli.”
“Kama Arsenal watafanikiwa kufanya hivyo na kushinda 1-0, basi watakuwa wamefanya kazi kubwa sana. Lakini naamini itakuwa vigumu sana kutoruhusu bao dhidi ya PSG. Kwa hiyo, inaweza kuisha 3-0 au 4-0 kwa PSG, au 1-0 kwa Arsenal.”


