Ufaransa ilianza kampeni yake ya Kombe la Dunia 2026 kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Senegal, ikichochewa na kiwango cha kipekee cha nahodha wake Kylian Mbappé, aliyeweka rekodi mpya ya ufungaji, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa MetLife siku ya Jumanne.

Mbappé aliifungia Ufaransa mabao mawili, na kufikisha jumla ya mabao 58 katika timu ya taifa, akivunja rekodi ya awali ya ufungaji ya muda wote ya nchi hiyo
Nyota huyo wa Real Madrid alifungua ukurasa wa mabao mapema kipindi cha pili kabla ya kuongeza bao la kuvutia mwishoni mwa mchezo na kuhitimisha ushindi. Mchezaji wa akiba Bradley Barcola pia aliandika jina lake kwenye orodha ya wafungaji wa Les Bleus.
Licha ya ushindi huo wa mabao 3-1, Ufaransa ilionekana kutokuwa katika kiwango chake katika kipindi cha kwanza. Senegal walitengeneza nafasi kadhaa hatari na walikaribia kupata bao kupitia Nicolas Jackson na Ismaila Sarr, lakini walishindwa kuzitumia vizuri nafasi hizo.
Baada ya mapumziko, Ufaransa walirejea wakiwa wamebadilika kabisa. Michael Olise alikuwa na mchango mkubwa katika mabadiliko hayo kwa kutoa ubunifu uliochochea safu ya ushambuliaji ya Wafaransa. Mbappé aliivunja ngome ya Senegal kwa kumalizia kwa utulivu kabla ya Barcola kuongeza bao la pili baada ya kuingia akitokea benchi.



