Uwanja wa Allianz Arena jijini Munich, Ujerumani, umechaguliwa kuwa mwenyeji wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2028, huku Camp Nou ya Barcelona, Hispania, ikipangiwa kuandaa fainali hiyo mwaka 2029. Uamuzi huo umetangazwa na Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) Jumanne, ukifungua ukurasa mpya wa historia kwa viwanja hivyo maarufu.
Kwa Allianz Arena, hii itakuwa mara ya tatu kuandaa fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya. Uwanja huo uliwahi kuwa mwenyeji mwaka 2012, wakati Chelsea ilipoifunga Bayern Munich kwa mikwaju ya penalti, kabla ya kuandaa tena fainali ya mwaka 2025 ambayo Paris Saint-Germain ilitwaa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bayern Munich, Jan-Christian Dreesen, alisema Munich iko tayari kutoa huduma bora kwa mashabiki watakaofika kushuhudia fainali hiyo. “Hii ni habari nzuri sana kwetu. Allianz Arena, Bayern Munich na Munich vinaashiria mvuto wa kimataifa, ukarimu wa kweli na kiwango cha juu cha maandalizi,” alisema Dreesen.
Kwa upande wa Camp Nou, fainali ya mwaka 2029 itakuwa mara ya tatu kwa uwanja huo kuandaa mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa. Mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1999, ambapo Manchester United iliifunga Bayern Munich kwa mabao 2-1 baada ya kufunga mabao mawili katika muda wa nyongeza.
Rais wa Barcelona, Joan Laporta, amesema klabu hiyo inajivunia kuaminiwa na UEFA kuandaa moja ya matukio makubwa zaidi katika soka la dunia. “Ni fahari kubwa kwa Barcelona na mashabiki wote wa Barcelona. Kuaminiwa na UEFA kuandaa moja ya matukio makubwa katika soka la dunia kunaonyesha ukubwa na matarajio ya mradi huu,” alisema Laporta. Kwa sasa, Camp Nou inaendelea na maboresho makubwa yaliyoanza mwaka 2023, huku fainali ya msimu wa 2026/27 ikiwa tayari imepangwa kufanyika Estadio Metropolitano, nyumbani kwa Atletico Madrid, Juni 5.


