Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limefungua rasmi kesi ya kinidhamu dhidi ya wachezaji wa Fenerbahçe, Matteo Guendouzi na Mason Greenwood, kufuatia tukio lililotokea katika mchezo wa marudiano wa mchujo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Olympique Lyonnais.
Guendouzi na Greenwood wanadaiwa kufanya ishara za kuwachokoza mashabiki wa Lyon wakati wa mchezo huo. Baada ya Fenerbahçe kushinda kwa mabao 2-1 mwezi uliopita, kulitokea vurugu wakati Guendouzi akitoka uwanjani, hali iliyosababisha UEFA kuanza uchunguzi dhidi ya wachezaji hao.
“Klabu yetu itawasilisha utetezi unaohitajika mbele ya vyombo husika vya UEFA ili kulinda haki na maslahi ya wachezaji wetu pamoja na Fenerbahçe katika mchakato huu,” klabu hiyo ya Uturuki ilisema katika taarifa yake.
Fenerbahçe pia imethibitisha kuwa yenyewe ipo chini ya uchunguzi wa UEFA kutokana na matukio yaliyojitokeza katika mchezo huo. Msemaji wa UEFA alisema: “Kila kitu kilichotokea katika mchezo huo bado kiko mbele ya chombo cha kinidhamu.”
Pamoja na sakata hilo, Fenerbahçe ilifanikiwa kutinga hatua ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuifunga Lyon kwa mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2 katika michezo miwili.


