Timu ya taifa Morocco imefanikiwa kuweka historia kwenye michuano ya kombe la dunia baada ya kuitupa nje timu ya taifa ya Ureno kwa kuifunga bao moja kwa bila katika mchezo wa robo fainali michuano ya kombe la dunia.
Ni katika Uwanja wa Al Thumama ambapo Historia ya Morocco na historia ya Afrika iliandikwa baada ya timu ya kwanza ya Afrika kufuzu nusu fainali ya michuano ya kombe la dunia ikiwatoa moja ya vigogo wa soka duniani timu ya taifa ya Ureno inayoongozwa na Cristiano Ronaldo.Alikua ni Youssef En Nesyri aliyeipatia bao la ushindi Simba wa milima ya Atlas dakika ya 42 ya mchezo na kuweza kudumu mpaka mchezo unamalizika na kuwatupa nje timu ya taifa ya Ureno kwenye michuano ya kombe la dunia na kufanikiwa kuweka historia.
Timu ya taifa ya Morocco walionekana kucheza kwa nidhamu kubwa sana kuanzia mchezo unaanza mpaka unamalizika huku wakizuia kwa umakini mkubwa sana na kufanya mashambulizi ya kushtukiza kwenye lango la timu ya taifa ya Ureno.Hatimaye historia kubwa imeandikwa kwenye taifa la Morocco na bara la Afrika baada ya timu hiyo kufanikiwa kua timu ya kwanza kutoka barani Afrika kufuzu nusu fainali ya michuano ya kombe la dunia.