Mabao mawili mazuri kutoka kwa Morgan Rogers, kila upande wa bao la kusawazisha la Cunha, yaliipa timu ya Unai Emery pointi zote tatu kwenye Uwanja wa Villa Park.
Manchester United wanaweza kuonekana kama hawakuwa na bahati kidogo kutopata chochote katika mchezo huo, baada ya kucheza vizuri kwa vipindi vingi dhidi ya Aston Villa walioko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.
Aston Villa bado wako nyuma kwa pointi tatu dhidi ya vinara Arsenal kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, huku wakiendelea kujijengea sifa kama wapinzani wa kweli wa kuwania ubingwa wa EPL.
Wakati huo huo, Manchester United walioko nafasi ya saba wanaendelea kuonyesha matokeo yasiyo thabiti chini ya kocha Ruben Amorim, licha ya kuimarika kwa kiwango cha uchezaji. Hadi sasa msimu huu wa EPL, United wana ushindi saba, sare tano na vipigo vitano.

Cunha anatarajiwa kuwa mchezaji muhimu kwa Manchester United katika mwezi ujao, hasa wakati Bryan Mbeumo na Amad Diallo watakapokuwa wakishiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Keane alivutiwa sana na kiwango cha mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil dhidi ya Aston Villa, na kumtaja kama “mchezaji halisi wa kiwango cha juu”.
Alipoulizwa kama anaona kipaji kwa Cunha, Keane alisema kupitia Sky Sports: “Hii ni zaidi ya kipaji, yeye ni mchezaji kamili. Hakukuwa na shaka kabisa kuhusu bao lile, ilikuwa ni kumalizia kwa kiwango cha juu. Halafu anakosa nafasi ya wazi kipindi cha pili kwa namna isiyoelezeka, ni vigumu kuelewa alivyoikosa.”

Licha ya United kucheza vizuri, Keane hakuwa na huruma nao, akiongeza hawezi kusema walikuwa na bahati mbaya waliruhusu mabao mawili. Wameruhusu mabao sita katika mechi mbili zilizopita na hilo halikubaliki. Wanawasifu kwa uwezo wao wa kushambulia na kweli sasa wanatengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini kwa idadi ya nafasi na mabao wanayoruhusu, huwezi kupiga hatua mbele.
“United wanaweza kupambana na kuonyesha moyo, walifanya hivyo tena leo, lakini wanahitaji kuwa makini na wenye nguvu zaidi wanapokuwa wanajilinda. Wanahitaji kuonyesha fahari zaidi upande wa ulinzi.”