Hesabu za Kocha Mkuu wa Azam FC raia wa DR Congo, Florent Ibenge ni kutengeneza hadithi tamu na ya kukumbukwa daima ndani ya timu hiyo kutoka mitaa ya Chamanzi.

Ibenge amebakiza dakika 90 tu kuandika historia hiyo ambayo haijawahi kutokea ndani ya timu hiyo tangu kuanzishwa kwake, takribani miaka 20 sasa.
Azam FC, imeanza vyema tiketi ya kuisaka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo, KMKM kutoka Zanzibar.
Katika mechi hiyo ya kwanza iliyopigwa Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, mabao ya Azam yalifungwa na mshambuliaji, Jephte Kitambala Bola dakika ya 6, huku lingine likifungwa na beki wa kushoto wa kikosi hicho, Pascal Msindo kunako dakika ya 42.
Timu hizo zitarudiana Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, kama wakishinda au kupata matokeo chanya watakuwa wamefuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza kwenye historia yao.



