Ukipiga simu kwenye uongozi wa klabu ya Yanga kuuliza nini mustakabali wao juu ya nani atakuwa kocha mkuu ajaye baada ya Roman Folz kuondoka, utachoambulia ni kuwa mchakato unaendelea na huku mtaani taarifa zikiwa Romuald Rakotondrabe ‘Roro’ ndiye amekuwa tageti kuu.

Ukweli ni kwamba Yanga wameanza upya mchakato wa kutafuta kocha wa timu hiyo baada ya mmoja wa viongozi kuweka wazi kuwa uwezekano wa kumchukua kocha Roro aliyekuwa anakaribia kutua katika timu hiyo, bila kutaja sababu za dili hilo kusuasua.
Uamuzi huo unakuja baada ya Yanga kuachana na aliyekuwa kocha wao Romain Folz, baada ya timu hiyo kupoteza mechi ya kwanza msimu huu ikifungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Silver Strikers ya Malawi yenye kiungo bora Uchizi Vunga.
Mechi hiyo ya mkondo wa kwanza hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imeiweka Yanga kwenye nafasi ya kutakiwa lazima ishinde angalau kwa tofauti ya mabao 2-0 katika mechi ya marudiano itakayopigwa Oktoba 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.
Folz ambaye ameiongoza Yanga kwenye mechi sita za mashindano, ameshinda nne na sare moja, timu yake ikifunga mabao tisa huku bao pekee ililoruhusu Malawi ndio lililohitimisha maisha yake ndani ya klabu hiyo, akichukua taji moja la Ngao ya Jamii.



