Mchezaji wa Juventus, Kenan Yildiz, ametuma salamu za heri kwa Igor Tudor, aliyefutwa kazi kama kocha mkuu wa Juventus siku ya Jumatatu, akisema: “Kila la heri kwa siku zijazo.”

Juventus walithibitisha rasmi kuachana na Tudor kama kocha mkuu baada ya mfululizo wa michezo minane bila ushindi katika Serie A na Ligi ya Mabingwa. Kikosi hicho cha Bianconeri hakikushinda tangu walipoibuka na ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Inter mnamo Septemba 13, na hakikuweza kufunga katika mechi nne za mwisho chini ya uongozi wa Tudor.
Kocha huyo raia wa Kroatia ndiye meneja wa kwanza kufutwa kazi katika Serie A msimu wa 2025-26, akiondolewa baada ya michezo minane pekee ya ligi.
Gleison Bremer alikuwa wa kwanza kati ya wachezaji wa Juventus kutoa shukrani kwa Tudor baada ya habari za kufutwa kwake kusambaa Jumatatu. Kupitia ukurasa wake wa Instagram Yildiz aliandika,“Asante kwa kila kitu, kocha. Nakutakia mafanikio katika siku zijazo.”



