Kocha wa England, Thomas Tuchel, ametuma ujumbe mzito kwa kiungo wake nyota Jude Bellingham, akisisitiza kuwa mchezaji huyo lazima aheshimu maamuzi ya benchi la ufundi hata pale yanapomkera. Hili limekuja baada ya Bellingham kuonyesha wazi kukasirishwa na kutolewa uwanjani katika ushindi wa 2–0 dhidi ya Albania kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia.
Bellingham, aliyekuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya kuanza na England tangu Juni, alipata kadi ya njano dakika ya 80. Tuchel hakutaka kuhatarisha hali hiyo, na dakika nne baadaye alimtoa ili kuzuia hatari ya kupewa kadi nyekundu, hasa wakati England tayari walikuwa wanaongoza.
Hata hivyo, kiungo huyo wa Real Madrid hakuona mambo hivyo. Kamera zilimnasa akipandisha mikono juu kwa hasira baada ya kuona Morgan Rogers akimsubiri ili aingie.
Baada ya mechi, Tuchel hakuwa na papara ya kuficha msimamo wake: “Huo ndio uamuzi, na lazima aukubali,” alisema.
“Rafiki yake anasubiri pembeni ya uwanja, hivyo unapaswa kuukubali, kuuheshimu na kuendelea mbele.”
Kauli hiyo imeonyesha wazi kuwa kocha huyo hatavumilia mienendo ya kukiuka nidhamu hata kama inatoka kwa mchezaji nyota.
Tuchel pia alikiri kwamba bado atatathmini tukio hilo baada ya kuangalia video, akisema: “Nimeona hakufurahia. Sitaki kulikuza zaidi kwa sasa.”
Bellingham na Tuchel tayari wamewahi kuwa na maingiliano huko nyuma, hivyo tukio hili linakuja kama mwendelezo wa mvutano unaoweza kuwa changamoto kwa England kuelekea 2026.
Licha ya tukio hilo, Tuchel alitumia muda kuwasifu wachezaji wake kwa kampeni ya kipekee ya kufuzu, waliyoikamilisha kwa kushinda mechi zote nane bila kuruhusu bao hata moja, ikiwa ni rekodi ya kihistoria barani Ulaya kwa timu iliyocheza angalau michezo sita.





