Baada ya uongozi wa Yanga kuweka wazi kuwa wameuchagua uwanja wa New Aman Complex uliopo Unguja visiwani Zanzibar kwa ajili ya mechi zake za nyumbani za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wamefichua kuwa wameshaanza mipango ya kuhakikisha wanatoboa.
Yanga wanatarajia kuanzia nyumbani kati ya Novemba 21 na 22 dhidi ya AS Far Rabat ya Morocco, hivyo kwa hesabu za viongozi hao wameona muda ni sasa wa kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye mchezo wake wa kwanza wakiwa nyumbani kwa kupata alama tatu.

Baadhi ya mashabiki wa Yanga ni kama wameipokea ratiba ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa presha wakiona kama ni safari ngumu lakini uongozi huo umetoka hadharani na kutoa neno zito lenye kutia neno la matumaini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo, ameeleza kuwa ratiba hiyo wameipokea na sasa wanaanza hesabu za namna ya kukabiliana na mechi hizo sita.
“Unaweza kusema ni ratiba ngumu lakini sisi ni Yanga tunajua ubora wa wapinzani wetu lakini tutajipanga kukabiliana na timu moja kwenda nyingine bila unyonge.Tuna timu imara sana na hivi karibuni mmeona tumeboresha benchi letu la ufundi kwa kumleta kocha mkubwa, tuko kwenye afya nzuri ya kwenda kushindana.

“Tunakwenda kujipanga sawasawa, tutakutana na benchi la ufundi lakini yapo mambo yatakuwa hadharani na mambo mengine hayatakuwa wazi, sio kila taarifa ya kukabiliana na adui yako inatakiwa kufika kwa mpinzani.
“Mashabiki wetu hawatakiwi kutishwa, Yanga ni kubwa, wanaodhani tutaanguka, tunatakiwa kwenda kuwathibitishia kwa vitendo ukubwa wetu, kuna ratiba huko nyuma zilitoka tukaona tutashinda lakini tukakwama na kuna ratiba pia tuliziona ngumu baadaye tukatoboa.”


