Kocha mkuu wa Brazil, Carlo Ancelotti, ameibua mjadala baada ya kutoa sifa nzito kwa kijana wa Chelsea, Estevão, kufuatia kiwango chake cha juu katika ushindi wa 2–0 dhidi ya Senegal kwenye uwanja wa Emirates. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 18 aliendelea kung’ara kwa kufunga bao lake la nne katika mechi kumi tu za kikosi cha wakubwa cha Selecão.
Estevão amekuwa katika kiwango cha juu msimu huu akiwa na Chelsea, licha ya kutumika zaidi kama mchezaji wa kutokea benchi na kocha Enzo Maresca. Hata hivyo, kila mara anapopewa nafasi, ameonyesha ubora uliowafanya wengi wamuone kama nyota muhimu ya baadaye.
Kasi, utulivu, uwezo wa kumalizia na ubunifu wa kufungua mabeki vimeufanya ulimwengu wa soka kumtazama kama kipaji kipya kinachokuja kwa nguvu.
Baada ya mchezo dhidi ya Senegal, Ancelotti hakuacha nafasi ya mashaka kuhusu thamani ya kijana huyo.
“Estevão ana kipaji cha ajabu,” alisema. “Ana uwezo wa kumalizia, ana uwezo mkubwa na anafanya kazi kwa bidii sana. Kwa kumuangalia, naweza kusema Brazil ina uhakika wa siku zijazo.”





