Manchester United wanatarajiwa kuchelewesha uamuzi wowote kuhusu mustakabali wa Joshua Zirkzee hadi baadaye katika dirisha la usajili la Januari, vyanzo vimeiiambia ESPN, huku kikosi cha Ruben Amorim kikiwa kimeathirika na majeruhi pamoja na wachezaji waliokwenda kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Chaguo za Amorim zimepungua kutokana na kukosekana kwa Bryan Mbeumo, Amad na Noussair Mazraoui walioko AFCON, sambamba na orodha inayoongezeka ya majeruhi inayowahusisha Matthijs de Ligt, Harry Maguire, Bruno Fernandes na Kobbie Mainoo.
Hali hiyo ilimlazimu kocha wa United kuwapa debut za kikosi cha wakubwa wachezaji wenye umri wa miaka 18, Jack Fletcher na Shea Lacey, katika kipigo cha 2-1 dhidi ya Aston Villa Jumapili, pamoja na kumtumia beki Lisandro Martínez kama kiungo wa dharura kipindi cha pili.
Zirkzee, ambaye amekuwa akipata muda mdogo wa kucheza msimu huu, anawaniwa na klabu kadhaa zikiwemo West Ham na Roma.
AC Milan pia walikuwa wakimwangalia mshambuliaji huyo wa Uholanzi kabla ya kuelekeza nguvu zao kwa mshambuliaji wa Kijerumani wa West Ham, Niclas Füllkrug.
Vyanzo vimeeleza kuwa hadi sasa Manchester United bado hawajapokea mawasiliano ya moja kwa moja kutoka klabu yoyote.

Zirkzee anayethaminiwa na United kwa takribani pauni milioni 30.5 (dola milioni 47) yuko tayari kuchunguza ofa zozote zitakazowasilishwa Januari.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anatambua kuwa anahitaji kucheza mara kwa mara zaidi ili kuongeza nafasi yake ya kuitwa kwenye kikosi cha Uholanzi kuelekea Kombe la Dunia la majira ya kiangazi yajayo.
Hata hivyo, United wana wasiwasi kuwa kikosi tayari ni chembamba, na wameweka wazi kwa Zirkzee pamoja na mawakala wake kuwa bado ni sehemu muhimu ya kikosi cha Amorim, hata kama si mchezaji wa kwanza kila mara.
Wakati huo huo, Manchester United bado wapo kwenye mbio za kumsajili winga wa Bournemouth, Antoine Semenyo.
Mchezaji huyo ana kipengele cha kuvunja mkataba cha pauni milioni 65 kinachotumika katika siku 10 za mwanzo za dirisha la Januari.


