Matatizo yanaendelea msimu huu kwa mshambuliaji wa Juventus, Dusan Vlahovic, ambaye amelazimika kujiondoa katika majukumu ya kimataifa akiwa na Serbia.

Mshambuliaji huyo amekuwa na shida msimu wote kutokana na hali mbaya na masuala ya utimamu wa mwili, ambayo hayaonyeshi dalili za kutulia sasa msimu wa Serie A umekamilika.
Taarifa ya Shirikisho la Serbia ilithibitisha kwamba Vlahovic amejiondoa kwenye kikosi chini ya kocha Dragan Stojkovic kwa mechi zijazo.
Serbia itacheza na Jordan katika mechi ya kirafiki Juni 16, kisha itamenyana na Hungary Juni 20 katika mechi ya kufuzu kwa michuano ya EURO 2024.

Baada ya mashabiki wa Juve kuanza kukosa subira na Vlahovic, jeraha hili la hivi punde pia halikupokelewa vyema na mashabiki wa Serbia, ambao walisema kwamba siku chache zilizopita fowadi huyo alionekana likizoni huko Mykonos akiwa na mchezaji mpya aliyesajiliwa wa Real Madrid, Jude Bellingham.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 aliweza kufunga mabao 14 na kutoa pasi nne za mabao katika mechi 42 za kimashindano akiwa na jezi ya Juventus msimu huu.

