Mikutano ijayo ya Ligi ya Mabingwa kati ya Juventus na Galatasaray itaashiria kurejea kwa pamoja kwa Luciano Spalletti na Victor Osimhen, waliotwaa ubingwa wa Serie A wakiwa Napoli msimu wa 2022–23.

Juventus wamepangwa dhidi ya Galatasaray kwenye mchujo wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa siku ya jana, jambo lililoandaa mkutano kati ya kocha wa Bianconeri, Spalletti, na mshambuliaji wa vigogo hao wa Uturuki, Osimhen.
Chini ya miaka mitatu iliyopita, wawili hao walitwaa ubingwa wa kihistoria wa Serie A wakiwa Napoli ubingwa wa kwanza kwa Partenopei baada ya miaka 33.
Osimhen alichangia kwa kiwango kikubwa mafanikio hayo kwa kufunga mabao 26, yaliyomfanya kuwa Capocannoniere (mfungaji bora) wa Serie A msimu wa 2022–23.
Kwa ujumla, Osimhen alifunga mabao 49 na kutoa pasi za mabao 12 katika mechi 71 chini ya Spalletti kwenye Uwanja wa Stadio Maradona.
Mshambuliaji huyo wa Nigeria alifunga mara tano katika michezo sita ya Ligi ya Mabingwa akiwa Napoli chini ya kocha huyo Muitalia, pamoja na mabao manne kwenye Ligi ya Europa msimu wa 2021–22, na mabao 40 katika misimu miwili ya Serie A.


