Mohammed Kudus alikuwa amekuwa mchezaji muhimu kwa Tottenham Hotspur kufuatia uhamisho wake wa £55m kutoka West Ham United majira ya joto yaliyopita.

Mohammed Kudus huenda asicheze tena kwa Tottenham msimu huu. Tottenham wamethibitisha kuwa Mohammed Kudus amepata pigo jipya katika mchakato wake wa kurejea kutoka jeraha la paja (quad injury).
Nyota huyo wa Ghana hajacheza tangu alipotolewa mapema katika kipindi cha kwanza cha sare ya 1-1 dhidi ya Sunderland mwezi Januari.
Spurs walikuwa na matumaini kuwa Kudus angerudi kabla ya mechi za mwisho za msimu, wakianzia katika safari ya Jumapili dhidi ya Sunderland.
Hata hivyo, mchezaji huyo wa zamani wa West Ham huenda asicheze tena msimu huu, huku pia ushiriki wake katika Kombe la Dunia ukiwa mashakani.

Taarifa ya klabu ilisema: “Tunaweza kuthibitisha kuwa Mohammed Kudus amepata pigo katika mchakato wake wa kupona majeraha. Nyota huyo wa Ghana alipata jeraha kubwa la paja katika mchezo wetu wa Premier League dhidi ya Sunderland mwezi Januari.”
Alikuwa amerudi katika mazoezi ya pamoja na timu wiki iliyopita, lakini sasa atahitaji uchunguzi zaidi wa wataalamu na huenda akahitaji upasuaji. Tutaendelea kutoa taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana. Ilisima taarifa hiyo.
Kutokuwepo kwa Kudus ni pigo kubwa kwa timu hiyo ya London, ambayo iko pointi moja tu juu ya eneo la kushuka daraja kabla ya mchezo wa wikendi kutokana na msururu wa mechi 13 bila ushindi.
Roberto De Zerbi tayari anakabiliwa na orodha ndefu ya wachezaji majeruhi kuelekea mchezo dhidi ya Sunderland.
Guglielmo Vicario alifanyiwa upasuaji wakati wa mapumziko ya kimataifa kutokana na tatizo la hernia, huku Dejan Kulusevski, Wilson Odobert, Ben Davies na James Maddison wote wakiwa majeruhi wa muda mrefu, ingawa Maddison yuko karibu kurejea.
Pape Sarr, Mathys Tel na Rodrigo Bentancur pia wanatiliwa shaka, huku Bentancur akiwa ameumia misuli ya nyuma ya paja katika kipigo cha 3-2 dhidi ya Bournemouth mapema mwaka huu.