Chelsea wanataka kumuuza Alejandro Garnacho chini ya mwaka mmoja tangu walipomsajili kutoka Manchester United, kwa mujibu wa talkSPORT.

Maisha ya Garnacho ndani ya Manchester United yaliharibika baada ya kauli zake hadharani kuhusu nafasi yake katika fainali ya UEFA Europa League. Kufuatia hilo, aliyekuwa kocha wakati huo Ruben Amorim anaripotiwa kumwambia kuwa afadhali aombe apate klabu ya kumsajili.
Chelsea walikuwa wakimfuatilia kwa muda na hatimaye walimsajili kwa pauni milioni 40, lakini mshambuliaji huyo wa pembeni hajafikia matarajio ya thamani yake, akiwa amefunga bao moja tu na kutoa pasi nne za mabao katika EPL msimu huu.
Kwa mujibu wa talkSPORT, Chelsea sasa wako tayari kumuuza Garnacho, wakifikia uamuzi huo chini ya mwaka mmoja tangu ajiunge na klabu hiyo. Inaelezwa pia kuwa uongozi wa klabu unakubaliana kwamba dili hilo halijaenda kama ilivyotarajiwa.
Hakuna taarifa rasmi ya bei ambayo klabu ya Stamford Bridge itakubali kwa sasa, lakini kutokana na kiwango chake kushuka, huenda wakalazimika kumuuza kwa bei ya chini kuliko waliyonunulia.


