Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema ana imani kubwa kuwa timu yao itafanya vizuri na hatimaye kurejesha heshima yake kwa kutwaa taji kubwa hapa nchini, licha ya kipindi kigumu walichopitia katika misimu ya hivi karibuni.
Amesema kwa msimu wa tano mfululizo Simba haijafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, sambamba na kushindwa kutwaa Kombe la Mapinduzi, lakini akasisitiza kuwa kila jambo lina wakati wake na mafanikio hayaji kwa pupa.
Ahmed amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa wavumilivu, akieleza kuwa ana uhakika Simba itarejea kwenye mstari wa ushindi na kunyakua kombe kubwa, licha ya kupoteza uhalisia wa kutwaa mataji kwa kipindi cha miaka mitano.
Akizungumza kuhusu ushiriki wa Simba katika Kombe la Mapinduzi, Ahmed alisema walikuwa na malengo mawili makubwa, ikiwemo kumpa nafasi kocha mkuu Steve Barker kuwajua wachezaji wake na mfumo wa timu.




