Atletico Madrid wamepoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya timu dhaifu Elche CF, ikiwa ni kipigo chao cha saba katika mechi nane zilizopita katika mashindano yote.

Wakiwa washiriki wa nusu fainali ya UEFA Champions League na watakaokutana na Arsenal Jumatano ijayo barani Ulaya, Atlético Madrid hawakuweza kujiimarisha baada ya kupoteza fainali ya Copa del Rey kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Real Sociedad wiki iliyopita.
Kocha Diego Simeone aliamua kutumia kikosi cha akiba zaidi ili kuwapa mapumziko wachezaji wake nyota baada ya mechi hiyo ngumu ya fainali, huku timu yake ikiwa tayari iko salama katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa La Liga.
Nicolas González alifunga mabao mawili kwa Atlético Madrid, lakini Elche walishinda kupitia mabao mawili ya André Silva na moja la David Affengruber, ushindi uliowasaidia kuongeza matumaini yao ya kubaki ligi kuu.
Mshambuliaji huyo wa Argentina alifungua ukurasa wa mabao baada ya pasi ya staili ya nyuma ya kisigino kutoka kwa Rodri Mendoza nje kidogo ya boksi.
Elche walirudisha bao kupitia Affengruber aliyesukuma mpira kuvuka Jan Oblak, na beki huyo huyo pia alihusika katika goli lililofuata la timu yake.


