FC Barcelona walisogea hatua moja karibu zaidi kutwaa ubingwa wa La Liga baada ya ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Celta Vigo jana, lakini wakampoteza mfungaji wao Lamine Yamal ambaye alionekana kupata jeraha la paja (hamstring).

Joao Cancelo pia alitoka uwanjani akiwa ameumia katika mchezo huo ambapo Barcelona walifanikiwa kuongeza pengo lao kileleni mwa msimamo hadi pointi tisa dhidi ya Real Madrid, wakiwa na mechi sita zilizosalia, ikiwemo mchezo wa El Clásico utakaochezwa Mei 10.
Kocha Hansi Flick aliwaongoza Barcelona katika mchezo wao wa kwanza tangu kutolewa kwenye robo fainali ya UEFA Champions League dhidi ya Atletico Madrid wiki iliyopita, lakini timu yake ilikosa ubunifu wa kawaida wa mashambulizi.
Kipa wa Barcelona Joan García alifanya save nzuri dhidi ya Pablo Durán na Ferran Jutglà katika dakika za mwanzo za mchezo.
Kwa kuwa kulikuwa na ushindani mdogo kati ya timu hizo, ilibidi kipaji cha Lamine Yamal kiwe ndicho kilichofungua mchezo. Mshambuliaji huyo aliingia ndani ya boksi, akicheza pasi fupi na Dani Olmo kabla ya kuangushwa na Yoel Lago alipokuwa akijaribu kumkwepa beki huyo wa Celta Vigo.

Yamal alifunga penalti ya chini na ya utulivu, akimshinda kipa Ionut Radu ambaye aliruka upande sahihi lakini hakuweza kuokoa.
Hata hivyo, baada ya kufunga bao hilo, Yamal alishika maumivu mara moja, akahitaji matibabu na akalala uwanjani wakati wachezaji wenzake wakisherehekea.
Mchezo huo ulisimama kwa zaidi ya dakika 15 kutokana na tukio la dharura la kiafya lililotokea kwenye jukwaa wakati huohuo, na baada ya mchezo kuanza tena, Yamal alikuwa tayari amebadilishwa na Roony Bardghji.
Barcelona walijitahidi kipindi cha pili bila kutengeneza nafasi nyingi za wazi hadi Ferran Torres alipofunga kwa volie nzuri kutokana na pasi ya Pedri, lakini bao hilo lilifutwa kwa sababu ya offside nyembamba.
Aliyekuwa beki wa Barcelona zamani Marcos Alonso alikosa kufunga kwa mpira wa adhabu uliogonga ukuta, lakini Barcelona walifanikiwa kushikilia ushindi muhimu.


