Herve Renard amethibitishwa kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya wanawake ya Ufaransa baada ya mgomo wa wachezaji uliopelekea kutimuliwa kwa Corinne Diacre.

Renard alijiuzulu wadhifa wake kama kocha wa Saudi Arabia mapema wiki hii, baada ya kusimamia ushindi wa kukumbukwa wa timu hiyo wa mabao 2-1 dhidi ya washindi wa Argentina katika Kombe la Dunia mwaka jana nchini Qatar.
Shirikisho la Soka la Ufaransa (FFF) lilimtimua Diacre mapema mwezi Machi baada ya wachezaji kadhaa wenye majina makubwa ya Bleues kukataa kucheza chini yake, wakikosoa mtindo wake wa usimamizi na jinsi anavyokishughulikia kikosi.
Renard alitajwa mara moja kama anayeweza kuchukua nafasi ya Diacre, na uteuzi wa kocha huyo wa miaka 54 ulikamilika hapo jana.

Mkataba wake na Les Bleues utaendelea hadi Agosti 2024, ukimruhusu kuiongoza timu hiyo kwenye Kombe la Dunia lijalo nchini Australia na New Zealand, na vile vile Michezo ya Olimpiki ya nyumbani mwaka ujao huko Paris.
Mbali na kuziongoza Zambia na Ivory Coast kunyakua taji la Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 2012 na 2015 mtawalia, Renard pia amechukua jukumu la Angola na Morocco katika maisha yake ya soka ya kimataifa.
Taarifa kutoka kwa FFF ilisema Renard atawasilishwa rasmi katika mkutano na waandishi wa habari siku ya leo, wakati pia atakapotaja kikosi chake kwa ajili ya mechi za kirafiki mwezi ujao dhidi ya Colombia na Canada.

Ufaransa wataanza kampeni zao za Kombe la Dunia dhidi ya Jamaica mjini Sydney Julai 23, kabla ya kumenyana na Brazil na Panama katika mechi zao za Kundi F.

