Atletico Madrid na kocha wao Diego Simeone mara kwa mara wameonja uchungu wa kushindwa, hata katika kile kinachochukuliwa kuwa enzi ya mafanikio makubwa ya klabu hiyo.

Atletico Madrid watakuwa wenyeji wa Arsenal kesho katika hatua ya nusu fainali ya UEFA Champions League, wakitafuta kurekebisha makosa yao baada ya kupoteza kwa maumivu katika fainali ya Copa del Rey wiki moja iliyopita.
Mashabiki makumi ya maelfu wa Atletico walisafiri kwenda Seville lakini wakarejea mikono mitupu, kama ilivyotokea pia katika fainali za UEFA Champions League za 2014 na 2016 dhidi ya mahasimu wao wakubwa Real Madrid.
Atletico hawajawahi kutwaa taji la juu kabisa la Ulaya, pia wakifungwa katika fainali yao nyingine ya mwaka 1974.
Wanaweza kuchukua hatua ya kwanza kuelekea fainali ya nne dhidi ya kikosi cha Arsenal wiki hii, ambapo klabu hiyo inaadhimisha miaka 123 tangu kuanzishwa kwake.
Katika mchezo wao wa kwanza nyumbani baada ya maumivu ya fainali ya Copa, Jumamosi dhidi ya Athletic Bilbao, mashabiki wa Atletico waliipokea timu yao kwa ubaridi.

“Mashabiki hawahitaji ujumbe (kutoka kwangu), wanachohitaji ni kushinda,”alibainisha kocha Diego Simeone akiwa Seville.
Hata hivyo kufikia mwisho wa ushindi wa 3-2 dhidi ya Athletic, ambao ulikuwa ushindi wao wa pili katika mechi tisa za mwisho katika mashindano yote, hali ilianza kubadilika.
“Tunahitaji kuinuka kutoka kwenye pigo hilo na kutoa kila kitu ili tufike fainali,” alisema mshambuliaji muhimu Julián Álvarez Jumatatu.
Mechi dhidi ya Arsenal inatoa njia ya haraka ya kujisafisha, na kufikia Jumatano mazingira yatakuwa ya moto na msisimko mkubwa, kama ilivyokuwa katika kuiondoa FC Barcelona kwenye robo fainali.
Atletico si tena kwenye uwanja wa Vicente Calderon, lakini uwanja wa Metropolitano Stadium ni wa nguvu sawa, hata zaidi kwa kelele kutokana na uwezo wake mkubwa wa mashabiki.
Uwanja huo uliofunguliwa mwaka 2017 haujafikia historia ya ule wa zamani, lakini hilo litachukua muda na utendaji mkubwa katika usiku kama huu kujengwa.
“Atletico wamehangaika kufika nusu fainali na fainali za UEFA Champions League. Tumejenga mafanikio haya kupitia kazi ngumu na msaada wa mashabiki wetu. Tunahitaji sasa zaidi kuliko wakati mwingine wowote, na tunatumaini tunaweza kuwapa wanachotaka uwanjani.“ Alieleza kocha huyo.

Pindi mazingira yanapokuwa sahihi katika uwanja wa Metropolitano Stadium, Atletico Madrid wameonyesha wanaweza kuivunja timu yoyote.
Walishinda FC Barcelona 4-0 katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Copa del Rey, ushindi uliokuwa mgumu kubatilishwa, na pia waliicharaza Real Madrid 5-2 kwenye derby mapema msimu huu.
Mechi hizo, pamoja na nyingine nyingi, zinapaswa kuondoa dhana kwamba timu ya Simeone hucheza soka la kujilinda tu na la polepole, ambalo lilikuwa msingi wa mafanikio yao mwanzoni mwa kipindi chake cha miaka 14.
Lakini jambo lisilobadilika kwa Simeone ni nguvu, juhudi na ushindani wa timu yake, pamoja na uwezo wa kuvumilia presha dhidi ya wapinzani wakubwa.
“Tumefika hapa kwa kushindana jinsi tulivyofanya hakuna kitu kilichotuzuia hadi sasa,” alisema Simeone.
Kushinda dhidi ya Athletic kunaweza kuwa chachu ya morali ambayo timu ilihitaji kuelekea mchezo dhidi ya Arsenal. Ni vizuri kushinda tena baada ya kipindi kigumu,” alisema Antoine Griezmann, ambaye anatarajiwa kuondoka klabuni majira ya kiangazi kwenda MLS na Orlando City SC.


