Massimiliano Allegri anaamini bado kuna nafasi ya kuboresha kwa kikosi chake cha Milan, licha ya kupata ushindi wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Bologna bila ya Rafael Leao, Christian Pulisic na Alexis Saelemaekers usiku wa jana.

Rossoneri waliendeleza rekodi yao ya kutopoteza katika Serie A hadi kufikia mechi 22 mfululizo, shukrani kwa mabao ya Ruben Loftus-Cheek, Christopher Nkunku na Adrien Rabiot katika ushindi huo wa 3-0 uliopatikana kwenye Uwanja wa Dall’Ara jana.
Akizungumza na DAZN baada ya mechi, Allegri alieleza kuwa Milan walicheza vizuri kwa sababu waliweza kunufaika na ushirikiano wa washambuliaji Nkunku na Loftus-Cheek, ambao hawakuwa wamewahi kuanza pamoja safu ya ushambuliaji kabla ya mechi ya jana.
“Nkunku na Loftus-Cheek ni wachezaji wenye ubora mkubwa sana. Ilikuwa lazima tuchukulie mechi hii kwa umakini, kwa sababu Bologna wana safu nzuri ya ulinzi. Ni timu hatari inayocheza vizuri. Wachezaji walifanya vizuri katika ulinzi na pia kwenye mashambulizi.” Alisema Allegri


