Ingawa Arsenal huenda walipoteza pointi katika mchezo wao wa mwisho wa EPL, bado zipo sababu nyingi za mashabiki na wadau wa klabu hiyo kuwa na furaha.

Bado wanaongoza ligi kwa tofauti ya pointi nne tofauti ambayo inaweza kuongezeka hadi saba katikati ya wiki na sasa wamefanikiwa pia kumbakisha nyota wao muhimu kwa mkataba mpya.
“Star boy” kama anavyojulikana kwa jina lake la utani, Bukayo Saka amesaini mkataba wa miaka mitano, hatua inayothibitisha thamani yake ndani ya kikosi. Nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza si tu amelipwa vizuri kwa mchango wake wa awali, bali pia amepewa motisha ya ziada kuendelea kutoa kiwango cha juu uwanjani.
Iwapo tutaangalia thamani ya kifedha, Saka sasa atalipwa pauni 300,000 kwa wiki, kiwango kinachomfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi ndani ya kikosi cha sasa cha Arsenal. Hii ni ishara ya wazi ya imani kubwa ambayo klabu imeweka kwake kama mhimili wa sasa na wa baadaye wa timu.
Habari za mkataba mpya wa Saka haziongezi pointi kwenye msimamo wa ligi, lakini zinaondoa usumbufu wowote ambao ungeweza kujitokeza. Wakati Arsenal wakiwa bado kwenye mbio za kuwania hadi mataji manne makubwa mwishoni mwa msimu, jambo la mwisho wanalohitaji ni kuvurugika kwa umakini wa kikosi.

Ingawa Saka hajawahi kuonyesha dalili za kutaka kuondoka, kuchelewa kusaini mkataba mpya kabla ya ule wa awali kuisha mwaka 2027 kulikuwa kunachochea uvumi wa uwezekano wa kuhamia kwingine. Sasa uvumi huo umekatizwa kwa saini moja tu.
Akiwa tayari amefunga mabao saba katika mechi 33 msimu huu, Saka ataelekeza nguvu zake katika kuivuruga safu za ulinzi za wapinzani badala ya kujadiliana mezani na viongozi wa klabu.
Uamuzi huu unaonyesha dhamira ya Arsenal ya kuwalinda wachezaji wao muhimu. Msimu uliopita, wachezaji kama William Saliba, Gabriel Magalhães, Ethan Nwaneri na Myles Lewis-Skelly pia walisaini mikataba mipya ya muda mrefu. Hii ni ishara kwamba wachezaji wa sasa na wa kizazi kijacho wanaiona mustakabali wao ukiwa ndani ya dimba la Emirates.
Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal wana ndoto ya kujenga enzi mpya ya mafanikio. Hata hivyo, enzi hiyo itathibitika tu ikiwa wataanza kushinda mataji mara kwa mara. Ingawa ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Chelsea kwenye fainali ya FA Cup Final mwaka 2020 ulikuwa mafanikio makubwa, mafanikio hayo yameonekana kufifia kadri muda unavyokwenda.


