Klabu ya Manchester City wako tayari kumuuza Jack Grealish ili kupata fedha za kumnunua Jude Bellingham wa Borrusia Dortmund.

Grealish ambaye ana miaka 27, alijiunga na Citizens kwa ada ya rekodi ya Uingereza ya pauni milioni 100 mnamo Agosti 2021 lakini ana mabao manne pekee na asisti tatu katika mechi 34 za Primia Ligi ndani ya kikosi cha Pep Guardiola.
Mchezaji huyo wa zamani wa akademi ya Aston Villa amecheza nafasi ya pembeni kwa Uingereza kwenye Kombe la Dunia, akipata dakika 55 pekee za mchezo katika michezo mitatu ya hatua ya makundi ya Three Lions.
Football Insider inadai Grealish sasa anaonekana kama mali inayotumika na wakuu wa Etihad, ambao watamweka mchezaji huyo kwenye soko la uhamisho ili kupata pesa ya kumnunua Bellingham.

Bellingham, 19, anaonekana kuwa mmoja wa vijana wenye vipaji vya hali ya juu zaidi barani Ulaya akivivutia vilabu vingi ikiwemo City, na ana uwezekano wa kuondoka Bundesliga msimu ujao wa joto.
Ingawa vyombo vya habari vya Ufaransa vinaihusisha sana Paris Saint-Germain na kutaka kumnunua kiungo huyo wa kati wa Uingereza, City wanajiandaa kufikia bei yake ambayo inatarajiwa kuvunja rekodi iliyolipwa kwa Grealish.
Bellingham ameanza mechi zote tatu akiwa na Uingereza huko Qatar na amefunga mabao tisa katika mechi 22 alizoichezea Dortmund hadi sasa, ingawa mkataba wake na wababe hao wa Ujerumani hautaisha hadi 2025 lakini anatarajiwa kuondoka Signal Iduna Park mwishoni mwa msimu.


