Aston Villa ya Unai Emery waliibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Bologna kwenye Villa Park, na hivyo kuhakikisha ushindi wa jumla wa mabao 7-1.

Kocha wa Aston Villa, Unai Emery, anatazamia kwa hamu nusu fainali “maalum” ya Europa League dhidi ya Nottingham Forest baada ya ushindi huo wa jana.
Villa waliingia kwenye mechi wakiwa na morali kubwa baada ya ushindi wa 3-1 katika mechi ya kwanza, huku Ollie Watkins akifungua ukurasa wa mabao kipindi cha kwanza kwa kufunga bao lake la 13 msimu huu na la tatu kwenye mkutano huo.
Emi Buendía aliifanya iwe 2-0 chini ya dakika moja baada ya Morgan Rogers kukosa penalti, lakini baadaye alijirekebisha kwa kufunga bao lililowafanya wenyeji waongoze 3-0 kabla ya mapumziko.
Ezri Konsa alifunga bao lake la pili kwenye mkutano huo na kukamilisha ushindi mkubwa mwishoni mwa mchezo.

Villa sasa wamepanga kukutana na Vítor Pereira na kikosi chake cha Nottingham Forest katika nusu fainali ya timu za EPL wakipigania nafasi ya kucheza fainali itakayofanyika Istanbul.
Timu hizi mbili zilikutana wiki iliyopita na kutoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa City Ground. Unai Emery alisema: “Ni muhimu kwa timu zote mbili na tuna kitu kinachofanana, klabu zote zimewahi kushinda Kombe la Ulaya. Wamekuwa na nyakati zao Ulaya kwenye kiwango cha juu katika historia yao, kama ilivyo kwa historia yetu pia.”
Kucheza nusu fainali ni muhimu sana kwao . Itakuwa nusu fainali nzuri sana kwa timu zote na mashabiki, na wanafurahia jinsi wanavyocheza. Wanajaribu kuthamini kila wakati pamoja na mashabiki wao kama leo Villa Park, wakiwa na shauku na motisha.
“Nusu fainali hii ni kitu maalum kwa timu zote mbili kwa sababu ni nafasi ya kucheza hatua hii, na najua ni vigumu sana kufika na kucheza nusu fainali.”
Emery pia alifurahishwa na namna timu yake ilivyomaliza mchezo mapema kwa mabao matatu ya haraka kipindi cha kwanza.
Aliongeza: “Leo tumetumia mpango ule ule wa mchezo kama tulivyofanya wiki iliyopita Bologna, tukiwaheshimu wao na mashindano. Kwa ujumla, kiwango cha uchezaji na kucheza mechi mbili kimekuwa cha kuvutia sana, lakini pia kigumu. Tumesinda mechi hii kwa matokeo makubwa, lakini ni kwa sababu tulicheza kwa umakini mkubwa.”
Unai Emery alisema walizungumza kuhusu kuanza kwa nguvu tofauti na wiki iliyopita na kuwa wakali zaidi katika eneo la mwisho (final third), na hilo ndilo lilifanya tofauti.

Ollie Watkins alifunga bao lake la 100 kwa klabu ya Aston Villa kupitia bao la kwanza la timu hiyo likiwa pia bao lake la nne kwenye mashindano haya msimu huu.
Mshambuliaji huyo wa Uingereza amekuwa na wakati mgumu kufunga katika vipindi fulani vya msimu huu, lakini Emery alisifu juhudi na kujituma kwake.
“Rekodi za binafsi ni muhimu kwa wachezaji. Leo ni siku maalum kwa Watkins kwa sababu amefanikisha hilo kupitia mafanikio ya timu, kwani tuko nusu fainali. Lakini pia tunataka kuwasaidia wachezaji kufikia malengo yao binafsi.”
Aliongeza: “Tunamhitaji Watkins kufunga mabao, kupata takwimu, hata kutoa pasi za mabao. Pia wachezaji wengine kama leo — Emi Buendía, Morgan Rogers, Ezri Konsa tunawahitaji nao wafunge. Lakini hasa tunapowasaidia wachezaji wetu kuboresha takwimu zao, washambuliaji ni muhimu sana. Leo ilikuwa siku ya Watkins.”

