Kipa wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Austria, Alex Manninger, amefariki dunia baada ya gari lake kuripotiwa kugongwa na treni mjini Salzburg siku ya jana.

Manninger alikuwa na umri wa miaka 48 na aliwahi kuchezea klabu kadhaa barani Ulaya, ikiwemo Juventus na Red Bull Salzburg. Klabu nyingi zilitoa salamu za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii.
“Tunaomboleza kifo cha kipa wetu wa zamani Alexander Manninger, ambaye amepoteza maisha kwa ajali ya barabarani. Mawazo yetu yako pamoja na familia na marafiki zake. Pumzika kwa amani, Alexander,” Salzburg waliandika kwenye X.
Polisi wa Salzburg hawakumtaja Manninger moja kwa moja, lakini shirika la utangazaji la taifa la Austria, ORF, liliripoti kuwa alijeruhiwa vibaya katika tukio lililotokea kwenye kivuko cha reli asubuhi ya jana.
Polisi walisema gari lilipigwa na treni na kuburutwa wakati likivuka reli. Dereva alikuwa peke yake ndani ya gari, huku dereva wa treni akiwa salama.
“Tarehe 16 Aprili majira ya saa 2:20 asubuhi, polisi waliitwa kwenye ajali ya barabarani iliyohusisha treni ya abiria na gari katika kivuko cha reli huko Nußdorf am Haunsberg,” polisi walisema.


