Roberto Martinez amemwambia Thomas Tuchel kwamba Anthony Barry atasalia kuwa sehemu ya wakufunzi wa Ureno hata kama aliondoka Chelsea na kwenda Bayern Munich.

Tuchel alifichua wakati wa kutambulishwa jana kama kocha mkuu mpya wa Bayern kwamba anatarajia kumuongeza Barry, ambaye alifanya naye kazi Chelsea, kama mmoja wa wasaidizi wake.
Barry anayeheshimika sana pia ametumia mwaka uliopita akifanya kazi pamoja na Martinez katika ngazi ya kimataifa, kwanza akiwa na timu ya taifa ya Ubelgiji na sasa Ureno.
Na bila kujali kama kocha huyo mwenye umri wa miaka 36 atasalia Stamford Bridge au atajiunga na Tuchel ya Ujerumani, Martinez anatarajia kubaki kama sehemu ya maandalizi yake ya ukufunzi.

Martinez amesema; “Nimekuwa na Anthony kwa miaka mingi. Kinachotokea katika soka ya kimataifa hakihusiani na soka la klabu. Kama kutakuwa na mabadiliko, yatakuwa kutoka klabu hadi klabu.”
Muda wa Martinez kama mkufunzi wa Ureno ulianza vyema kwa ushindi wa 4-0 dhidi ya Liechtenstein katika mechi ya ufunguzi ya kufuzu kwa Euro 2024 Alhamisi. Ureno ilipanga safu kali kwenye mchezo huo iliyomjumuisha Cristiano Ronaldo, ambaye alifunga mara mbili siku alipokuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika soka la kimataifa la wanaume.
Bernardo Silva pia alifunga bao, lakini amewaonya wachezaji wenzake kutowachukulia poa wapinzani wao wa Kundi J, Luxembourg, hata kama wako katika nafasi ya 92 duniani.

Silva alisema; “Ukweli ni kwamba hatujui nini cha kutarajia kwa sababu timu zinaweza kubadilika kulingana na wanavyoona kwenye michezo ambayo tumekuwa tukicheza na wanaweza kuzoea mchezo wetu. Tunatarajia mchezo mgumu, mara ya mwisho tulipokuja hapa tulipitia magumu mengi, timu imeimarika sana, kama sijakosea hawajapoteza katika mechi saba.”
Martinez bado anaendelea kukielewa kikosi chake, akiwa amechukua nafasi ya Fernando Santos miezi miwili iliyopita, na alipendekeza mabadiliko yatafanywa dhidi ya Luxembourg.
Kocha huyo amesema kuwa amekuwa pamoja na kikosi kwa siku tatu na amefurahishwa na kiwango cha umoja, matarajio na kujitolea kwa wachezaji,, ubora wa kikosi ni wa kipekee.

“Tuko mwanzoni mwa safari; tunapaswa kukua pamoja. Lakini daima ni rahisi unaposhinda. Ushindi wetu wa mwisho ulikuwa muhimu kwa mtazamo huo.”

